Home VIWANDAUZALISHAJI Uzalishaji mazao ya chakula waongezeka Mbinga

Uzalishaji mazao ya chakula waongezeka Mbinga

0 comment 72 views

Uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga (MTC) umeongezeka kwa asilimia 7.9 katika msimu wa 2022/23 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Afisa Kilimo na Msimamizi wa Pembejeo wa MCT Andrew Chiwinga amebainisha hayo Oktoba 24, 2023.

Ameeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na mfumo mzuri wa upatikanaji wa mbolea za ruzuku.

Chiwinga ameeleza kuwa katika msimu wa 2022/23 uzalishaji umeongeza kufikia tani 80,900 ikilinganishwa na tani 75,000 zilizozalishwa mwaka 2021/22.

“Mfumo wa mbolea za ruzuku umewasaidia wakulima kupata mbolea kwa bei nafuu na kwa wakati na hivyo kuongeza tija katika kilimo,” ameeleza.

Amesema kwa msimu uliopita walipokea mbolea tani 15,613 ikilinganishwa na matarajio ya tani 10,500.

Aidha, ameongeza kuwa ongezeko hilo lilitokana na Wilaya nyingine za Mbinga vijijini na Nyasa kuchukua mbolea kutoka Mbinga Mji.

Chiwinga amesema kwa Halmashauri ya Mji wa  Mbinga, mahitaji yao  ya mbolea yanakadiriwa kuwa tani 12,500 kwa mwaka 2023/24 ikilinganishwa na tani 10,500.

Amesema hiyo inatokana na kuongezeka kwa wakulima wanaojisajili katika mfumo wa mbolea ya ruzuku.

Amebainisha kuwa msimu uliopita waliweza kuwasajili na kuwaingiza kwenye mfumo wakulima 21,099  na kuwapatia namba za kununulia mbolea ya ruzuku.

Ili msimu huu wa 2023/24 wakulima wengi zaidi wanufaike na mbolea ya ruzuku aliwataka kwenda katika maeneo waliojiandikisha kuhakiki taarifa zao.

Chiwinga amesema mbali na uhakiki wa taarifa, pia usajili mpya kwa wale ambao hawakujiandikisha msimu uliopita unaendelea katika kata na vijiji vya MCT.

Mkulima katika Halmashauri hiyo Alex Saligo amesema hivi sasa  mbolea za ruzuku zinawasaidia sana wakulima tofauti na zamani ambapo kila muuzaji alikuwa anapanga bei yake.

Mkulima mwingine Erick Komba aameeleza kuwa baada ya serikali kuanza kutoa mbolea za ruzuku wameondokana na usumbufu kwa kuwa zinauzwa kwa bei elekezi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter