Home VIWANDAUZALISHAJI Vijana achaneni na miradi ya kawaida: Rais Samia

Vijana achaneni na miradi ya kawaida: Rais Samia

0 comment 224 views

Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza vijana wawe na fikra za mageuzi ya kiuchumi kwa kubuni na kuanzisha miradi badala ya kusubiri kuajiriwa au kutaka utajiri wa haraka.

Akizingumza wakati wa kuhitimisha matembezi ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuadhimisha miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar amewataka vijana kuja na mawazo mapya ambayo yana mahitaji sokoni.

“Nataka kuwaambia kazi ya serikali si kutengeneza ajira, ni kuweka mazingira mazuri ili vijana myatumie kutengeneza ajira. Na hiyo kazi tunaifanya vya kutosha. Naomba muende mkatengeneze ajira kwa mazingira yaliyopo.

Naombeni sana vijana kajengeni uchumi wa chini mtusaidie serikali, mkijipanga vizuri na kuja na mawazo mazuri fedha za kuwasaidia kujenga miradi yenu zipo,” amesisitiza Rais Samia.

Amesema kwa kufanya hivyo kelele za ukosefu wa ajira hazitakuwepo.

Ameeleza kuwa zipo fursa katika sekta za kilimo na uchumi wa buluu hivyo vijana wazichangamkie kwa kuwa serikali imeweka bajeti ya kutosha kwenye sekta za uzalishaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na nchi ipate maendeleo endelevu.

Amewataka vijana kuachana na miradi ya kawaida inayofanana na kuwa wabunifu na kusema “ukimuona mwenzio kaweka kiwanda cha tofali ni kiwanda cha tofali kila baada ya kilomita tatu au moja, kama ni duka ni maduka hujui nani ananunua, visaluni ni hivyo hivyo.”

“Vijana wa leo tunakimbilia kwenye kutaka utajiri. Uwe na nyumba nzuri, uwe na gari zuri, mambo yako yaende hivyo lakini baada ya muda utajiri ule unakugeuka unakupiga. Kama ni jumba zuri huwezi tena kulitunza, kama ni gari huwezi kulitunza unarudi tena kwenye unyonge,” amesema.

“Katika dhana ya uchumi wa buluu wanawake hapa Zanzibar wamefanikiwa kwa kuanzisha mradi wa mwani ambao unafanya vizuri lakini naamini vijana wangeweza kufanya miradi mingi zaidi na kuacha kufanya miradi ya kufanana kwa sababu rasilimali za bahari zipo,” amesema Rais Samia.

Ameutaja uvuvi wa vizimba kuwa ni fursa nyingine ambayo vijana wanaweza kuitumia kwani wapo wataalamu wa kutosha na kwamba wanaweza kuuza mazao ya samaki kwenye hoteli na kwa wananchi hivyo kujipatia kipato.

Aidha Rais Samia amewaonya vijana wasiopenda kujishughulisha na wenye tabia ya kutaka kufanyiwa kila kitu na kusema kuwa kuendekeza mienendo ya namna hiyo kutapelekea nchi kuuzwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter