Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Sima amesema serikali itahakikisha hakuna shughuli zozote za kilimo na kibinadamu katika vyanzo vinavyopeleka maji Mto Rufiji ili utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme katika bonde la mto huo ufanyike. Sima amesema hayo baada ya ziara yake katika mikoa sita, kwa ajili ya kukagua maeneo yanayokumbwa na changamoto mbalimbali za mazingira na kutafuta suluhisho.
“Ziara yangu imeanzia Lindi, Ruvuma, Njombe, Mbeya, Iringa na Kilombero kote huko nimelenga kujione vyanzo hivi vikuu. Mito hii ya Ruaha Mkuu, Kilombero na Luegu inapoungana ndio inatengeneza Mto Rufiji ambako ndiko kuna maporomoko ya “Stigler’s Gorge”. Na nimeridhishwa na hatua za watendaji katika ngazi zote za serikali kwa kuwa mstari wa mbele kukahikisha kuwa vyanzo vya maji vinalindwa na kuhifadhiwa”. Amesema Naibu Waziri huyo.
Pamoja na hayo, Naibu Waziri Sima ameeleza kuwa serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji wa Rufiji Hydro Power Project ambapo inatarajiwa kuwa takribani MW 2100 za umeme zitazalishwa.
“Uhifadhi wa mazingira katika Bonde la Rufiji ni wa faida kwa pande zote hasa ustawi wa wananchi. Wananchi ndio walinzi na wahifadhi wa kwanza katika kutunza mazingira, aidha Sheria ya Mazingira, 2004 kifungu cha 6 kimetamka wajibu wa kila mwananchi kutunza mazingira kwamba; Mtu yeyote anayeishi Tanzania atakuwa mdau na atawajibika kutunza na kuendeleza mazingira na kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu shughuli au jambo lolote ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mazingira. Hivyo kupitia Sheria hii, si jukumu la serikali pekee kusimamia uhifadhi wa mazingira, wananchi nao wana wajibu wa moja kwa moja wa kutunza mazingira”. Amesisitiza.