Wito umetolewa kwa wawekezaji wote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Iringa ambapo mkoa huo umebarikiwa kuwa na madini ya aina mbalimbali ikiwemo dhahabu, vito, chuma, madini ya viwandani na madini ya ujenzi.
Wito huo umetolewa na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Mhandisi AbdulRahman Milandu wakati akizungumza katika mahojiano maalum.
Mhandisi Milandu amesema “madini ujenzi yapo tele wawekezaji waje kuwekeza, pia tuna maeneo ya dhahabu kama Nyakavangala, Ifunda, Kitengulinyi, kijiji cha Sinai na Igoma Wilayani Mufundi yana fursa ya madini ya kutosha ya dhahabu hivyo wawekezaji wakubwa waje kuwekeza.”
Akizungumzia suala la makusanyo ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa huo yatokanayo na mrahaba, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ameeleza kuwa yamefikia shilingi milioni 698.05 ikiwa ni asilimia 58.2 ya lengo walilowekewa.
Mhandisi Milandu amebainisha kuwa Mkoa umewekewa lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 1.2.
“Mwaka huu wa fedha mpaka sasa tunakaribia asilimia 60, tumekusanya shilingi milioni 698.05 zaidi ya nusu ya lengo, hii inaonyesha fursa zipo, ameeleza.”