Na Mwandishi wetu
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema wakati akifungua tamasha la 14 la kijinsia ambalo limeandaliwa na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) kuwa, Tanzania imepata sifa kubwa katika mkutano wa Umoja wa Mataifa (AU) aliohudhuria kupitia Benki ya Wanawake na jitihada zake mbalimbali za uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Ameongeza kuwa serikali bado inaendelea kufanya michakato mbalimbali kama vile kuanzisha mifuko ya uwekezaji, vikoba na saccos ili kuwainua wanawake. Pia Makamu huyo wa Rais amesema serikali inalenga kuifufua benki ya wanawake ambayo kwa sasa inaonekana kulegelega ili isimame na kufanya kazi zake kwa malengo ambapo haitosaidia wanawake tu, bali hata wanaume watanufaika nayo.
Mbali na hayo, Samia ametoa agizo kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua dhidi ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii kwani vitendo hivi vimezidi kuongezeka hapa nchini. Ametaka Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Lazaro Mambosasa kuhakikisha vitendo hivyo vya ukatili vinakomeshwa hapa nchini.