Home WANAWAKE NA MAENDELEO Kwanini biashara za wanawake haziendelei?

Kwanini biashara za wanawake haziendelei?

0 comment 100 views

Wanawake wamekuwa mstari wa mbele kujiajiri kwa kuanzisha biashara zao na kwa kiasi kikubwa hii imesaidia suala ya kutegemea chanzo kimoja tu cha mapato katika familia. Licha ya hivyo, ukweli ni kwamba, kuanzisha biashara na kuendesha biashara ni vitu viwili tofauti. Wanawake wengi wamefanikiwa kuanzisha miradi yao lakini wachache sana wameweza kuendesha biashara zao kikamilifu hadi kuhakikisha zinafanikiwa.

Hivyo basi, kwanini wanawake wengi wanapata wakati mgumu kuendeleza biashara zao? Tatizo ni nini? Nini kinatakiwa kufanyika ili biashara hizi ziendelee? Ni wapi hasa wanawake wanakwama?

Hizi hapa ni sababu kuu 4 kwanini biashara nyingi za wanawake hufa.

Majukumu ya kifamilia

Wanawake wana majukumu mengi katika familia hivyo inakuwa ngumu kuendesha biashara kikamilifu kwani mara nyingi wanalazimika kushughulikia familia hususani watoto hivyo masuala ya biashara hayapewi kipaumbele ipasavyo. Majukumu mengi ya nyumbani muda mwingine hukwamisha wanawake kutumia muda mwingi zaidi kuhakikisha biashara inakwenda vizuri. Hii ni moja ya sababu kubwa wanawake huamua kuacha kufanya biashara kwani ni ngumu kufanya kila kitu kwa wakati mmoja.

Ili kukabiliana na changamoto hii, unaweza kuomba msaada kwa kushirikisha familia katika kugawa majukumu ili upate muda wa kutosha wa kuendesha biashara na kusimamia majukumu inavyotakiwa.

Elimu ya biashara

Kila biashara inahitaji maarifa na ujuzi. Mara nyingi, wanawake huanza biashara bila kujua wanachohitaji kuendesha biashara hiyo hivyo wanakosa elimu ya mambo muhimu kama vile namna ya kutunza fedha, jinsi ya kushawishi wateja, taarifa za biashara nk.

Mbali na kuwa na elimu ya darasani, elimu ya biashara ni muhimu kwani kuna baadhi ya vitu huwezi kufundishwa shuleni na unapokosa ufanisi na kukabiliana na changamoto nyingi zilizopo katika sekta ya biashara, ni rahisi zaidi kukata tamaa.

Ili kuwa katika nafasi nzuri zaidi, hakikisha unafanya utafiti wa kutosha kabla ya kuanzisha biashara yako. Jifunze kupitia semina ambazo huendeshwa bure sehemu mbalimbali, omba ushauri kwa wanawake wengine ambao wamekuwa wakifanya biashara kwa mudamrefu zaidi na pia tumia mtandao kupata maarifa zaidi.

Ubunifu

Asilimia kubwa ya wanawake hawatumii ubunifu wanapoanzisha biashara na badala yake, wanafanya maamuzi kutokana na yale wanayoona katika biashara nyingine. Kama mfanyabiashara ni muhimu kuwa mbunifu kwani utofauti wako ni moja kati ya kivutio kikubwa kwa wateja. Hakikisha unatumia ubunifu wako kujitofautisha sokoni na siku zote epuka kuiga na kufanya maamuzi kutokana na kile unachoona katika biashara nyingine.

Tamaa

Ni rahisi kwa wanawake kuvutiwa na vitu hata kama hawavumudu kifedha. Kutokana na hilo, wengi wao hujikuta wakitumia fedha za biashara kwa ajili ya mahitaji binafsi hivyo kupelekea biashara kuendeshwa kwa hasara na mwisho wake kufungwa kwa sababu faida haionekani. Ni muhimu kuangalia matumizi yako kwa karibu zaidi na kuwa na nidhamu ya fedha ili kufanikiwa katika biashara. Epuka kutumia fedha katika mambo yasiyo na mchango wowote katika kukuza biashara.

Japokuwa kuna vikwazo vingi kwa wanawake wafanyabiashara, inawezekana kabisa kupata mafanikio na kutimiza malengo yako. Endelea kujifunza kila siku na usikate tamaa hata pale mambo yanapokuwa magumu kupita kiasi. Tambua malengo yako na wekeza jitihada kubwa ili kuyatimiza.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter