Home WANAWAKE NA MAENDELEO Soko la ajira nchini liwapatie fursa zaidi wanawake

Soko la ajira nchini liwapatie fursa zaidi wanawake

0 comment 102 views

Tatizo la ajira sio jambo la kushangaza sehemu nyingi duniani. Ni suala ambalo watu wamefikia kuliona kama ni jambo la kawaida tu. Lakini unafahamu kwamba changamoto hii ni kubwa zaidi kwa jinsia ya kike kuliko ile ya kiume? Utafiti uliofanyika kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Walemavu kama alivyoeleza Joseph Nganga ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira katika ofisi hiyo unaonyesha kuwa, ni wanawake asilimia 11.4 waishiyo mijini wanakumbwa na changamoto ya ajira.

Lakini swali la muhimu la kujiuliza hapa ni, wanawake wanaosoma ni wachache kuliko wanaume? Kwanini wanaume wengi zaidi wanaajiriwa kuliko wanawake? Kwanini soko la ajira halina idadi sawa kati ya jinsia hizi? Tatizo ni nini?

Utafiti huo unaonyesha kuwa moja ya sababu kubwa ya wanawake kutoajiriwa ni ujuzi duni. Wanawake wanakuwa na elimu inayokubalika lakini kinachosaidia wanaume katika soko la jira ni kwamba wengi wao wanakuwa na elimu lakini pia na ujuzi hivyo waajiri huwachagua wao mara nyingi.

Katika jiji la Dar es salaam pekee, ukosefu wa ajira kwa wanawake unachukua asilimia 26. Unaweza kujiuliza jiji hili lina wanawake wangapi? Wanafanya nini kupambana na changamoto ya ajira? Wanategemea wanaume kiuchumi? Wanaendeshaje familia? Serikali inachukua hatua gani kuwasaidia?

Wanawake wengi hukimbilia katika ujasiriamali, biashara ndogondogo, kilimo cha mbogamboga na shughuli za kiuchumi katika vikundi ili kujikwamua na kujiondoa na umaskini. Lakini jitihada hizi pekee hazitoshi. Kundi hili linapaswa kupewa motisha na kufanya makubwa zaidi katika jamii. Milango ya ajira inapaswa kuwa wazi kwao ili wapate nafasi ya kufanya makubwa zaidi katika jamii.

Serikali inapaswa kutumia sauti iliyonayo na kuelimisha jamii kuhusiana na changamoto hii. Wanawake nao wasikate tamaa kuhusu ajira, waendelee kujiunga na vyuo vikuu na kufuata ndoto zao. Kama ajira ikishindikana wasiishie kulalamika tu wajiajiri, wawekeze na kujiendeleza kiuchumi. Wala wasikate tamaa na kuvunjika moyo. Wanawake ni kundi muhimu sana katika maendeleo ya jamii kote duniani hivyo wasikubali kuachwa nyuma.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter