Muasisi na mwenyekiti wa taasisi ya Dk Ntuyabaliwe, Jacqueline Mengi amezindua Maktaba ya Shule ya Msingi Tandale Magharibi na kutoa wito kwa wanafunzi kuitumia vyema maktaba hiyo kujenga maarifa.
Aidha amewataka wanafunzi kuilinda maktaba hiyo kama chanzo cha maarifa na weledi.
Maktaba hiyo imewezeshwa na taasisi hiyo kufuatia shindano la Andika Chalenge kwa shule za serikali nchini.
Aliwataka pia wazazi kutekeleza jukumu lao la kushawishi watoto kusoma vitabu na kutumia maktaba na kuwa weledi katika masomo kwa kujisomea.
Akizindua maktaba hiyo ambayo Taasisi iliikarabati, kuweka mashubaka pamoja na vitabu vya aina mbalimbali, Mwenyekiti wa Taasisi, Jacqueline Ntuyabaliwe Mengi amesema amejisikia furaha kutimiza ahadi ya kukabidhi maktaba kwa shule hiyo iliyotoa mshindi.
Katika shindano hilo la uandishi la Andika Challenge ambalo linafanyika mikoa yote Tanzania na kushirikisha wanafunzi wote wa shule za msingi za serikali kuanzia darasa la 4 mpaka la 7 ambapo wanafunzi huandika hadithi na kutuma kwa sanduku la posta 163 Dar es salaam, washindi huzawadiwa tuzo na shule aliyotoka husaidiwa kuwa na maktaba.
Shule ya Msingi Tandale Magharibi imepata maktaba hiyo baada ya mwanafunzi wake Nuurat Venance kushinda shindano la kutunga hadithi lililowashindanisha wanafunzi wa shule za msingi za manispaa za Kinondoni na Ubungo, jijini Dar es salaam. Hivi sasa shindano hilo linawashindanisha wanafunzi wote wa shule za msingi hapa nchini.
Alisema baada ya mshindi kupatikana mwaka jana ambaye alitoka katika shule hiyo, taasisi ilibaki na changamoto ya kuwezesha kupatikana kwa maktaba, na anapoifungua maktaba hiyo anafurahishwa kuwa taasisi imetekeleza ahadi yake kwa mshindi wa shindano hilo.
Jacqueline Mengi akizungumza katika makabidhiano hayo alisema kwamba nia kubwa wa shindano hilo ni kusaidia watoto kujua kusoma na kuandika na pia kuwa wabunifu na kutumia ubunifu wao kusonga mbele.
Alisema pamoja na serikali kuwezesha elimu bure, wao kama taasisi wanatoa mchango wao ambao utasaidia kuimarishwa kwa tabia ya kusoma na kujipatia maarifa kutoka katika maktaba.
Alisema taasisi ya Dk Ntuyabaliwe iliyoanzishwa kwa ajili ya kumuenzi baba yake ambaye alikuwa anapenda sana kujisomea vitabu na kuwahimiza watoto wake akiwemo yeye kujifunza kusoma, kwa sasa inaendesha shindano hilo la Andika Challenge ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wanajijenga katika ubunifu na matumizi wa lugha ya Kiswahili kwa kutunga hadithi zao wenyewe.
Anasema kwa msimu huu mashindano hayo yanaendelea na kwamba vigezo vinavyostahili kufanywa na wanafunzi kuanzia darasa la 4 hadi la 7.
Ikiamini kwamba kusoma na kuandika ndio njia pekee ya kukabiliana na wanafunzi wanaomaliza shule bila kujua kuandika Jacquline alisema kwa sasa wamewezesha shule 7 kuwa na maktaba, wanafunzi 4,406 kusaidia mambo mbalimbali na vitabu takaribani 20,827 kuwafikia wanafunzi.
Mapema Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Grace Mtesigwa alisema kitendo cha kukabidhi maktaba kwa shule hiyo, Taasisi ya Dk Mtuyabaliwe imekuwa ikiunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais John Magufuli za kuboresha elimu nchini.
Wakitoa shukrani kwa niaba ya shule, Mwalimu Mkuu Doris Msigalo na Mwakilishi wa Wazazi Sudi Makamba wameishukuru Taasisi na kusisitiza kuwa wataitumia na kuitunza vizuri maktaba hiyo.