Home WANAWAKE NA MAENDELEO Wanawake watakiwa kupata elimu ya fedha kabla ya mikopo

Wanawake watakiwa kupata elimu ya fedha kabla ya mikopo

0 comment 136 views

Wanawake wametakiwa kuacha kukimbilia kukopa fedha kabla ya kuwa na elimu ya fedha.

Kutokuwa na elimu ya fedha kunawasababisha kuishia kupata matatizo mbalimbali kutokana na madeni kwa kushindwa kulipa mikopo hiyo.

Beng’i Issa ambae ni Katibu  Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi kiuchumi (NEEC), ameyasema hayo na kudai kuwa sekta  ya fedha imekuwa ngumu huku watu wanataka kujikwamua kiuchumi lakini hawana elimu.

Amesema elimu ya fedha na biashara bado ni kikwazo kikubwa kwa wananchi kwani wengi wanashindwa kujikwamua kiuchumi licha ya kukopa  fedha lakini namna ya kuzitumia hawajui na kujikuta wakiingia katika mzigo wa madeni yasiyokuwa na tija.

“Wanawake wengi wamekuwa wakikopa fedha katika taasisi za kifedha ambazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kuwafilisi.”

Amesema, kinachofanyika baada ya kushindwa kulipa mkopo ni kuchukuliwa vitu vya ndani ikiwemo Kitanda, luninga, friji na vitu vingine.

Amebainisha kuwa mwaka jana (2022) kupitia mifuko ya uwezeshaji kiuchumi nchini, imetoa mikopo ya Sh trilioni 5.6 kwa  watanzania milioni 9.8 kati yao wanawake ni asilimia 53.

“Serikali iliona hili tatizo hasa vikoba vilipoanza mwaka 2000 na vilianza kupitia asasi za kiraia, watu wakawa wanajifanyia bila kuwa na sheria yoyote.

“Kwa sasa hiyo sheria imeanzishwa ya huduma ndogo za fedha, lakini bado tatizo ni kubwa na tatizo sisi tunalifahamu, ni elimu ya fedha inatakiwa kwa wanawake,”ameeleza.

Amesema, kwa sababu watu wengi sana wanataka kujikwamua kiuchumi, wanafikiri kujikwamua kiuchumi ni kwenda kuchukua mikopo.

“ Kuchukua pesa iwe ni kitu cha mwisho katika uwezeshaji, sisi tunasema kabisa unaweza kufanikiwa kufanya jambo lolote lile mradi una utashi, na ukafanikiwa kwa hela yako ndogo ambayo umeweka wewe mwenyewe.”

Aidha, amesema mikopo inawafanya watu wengi wavuke kibiashara yaani wapige hatua lakini uwe na uhakika wa kile unachokwenda kukifanya,  uwe na nidhamu ya huo mkopo.

Amesema “usichukue mkopo ukaenda kulipa ada ya shule utaurudishaje? Ukichukua mkopo ukaenda kununua bati kujenga nyumba, utarudishaje? “chukua mkopo ukafanye shughuli ya kiuchumi ambayo inakuingizia faida ili ukalipe ule mkopo.”

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter