Home KILIMO TMX: Suluhisho la wakulima Tanzania

TMX: Suluhisho la wakulima Tanzania

0 comment 172 views

Wewe ni mwekezaji, mfanyabiashara au mfanyakazi mwenye udhubutu ambaye unatamani fursa ya kuingiza kipato cha ziada? Haijalishi upo kundi gani, jibu lako ni soko la bidhaa. Bila shaka umewahi kusikia kuhusu Soko la hisa. Sasa natambulisha kwako Soko la bidhaa. Dhana ni ile ile lakini badala ya hisa, katika soko hili kuna bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mazao ya biashara, dhahabu na hata mafuta ghafi.

Kwa upande wa Tanzania, soko la bidhaa linaendeshwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) ikihusisha taasisi mbalimbali za serikali na zile zisizo za serikali. Aidha, imesajiliwa kama kampuni binafsi inayofahamika kama Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), soko la kwanza kabisa la bidhaa hapa nchini.

TMX ilizinduliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kassim Majaliwa katika maadhimisho ya siku ya wakulima (08/08) mwaka huu. Japokuwa ofisi za soko hili zinapatikana jijini Dar es salaam, huduma zinapatikana mtandaoni hivyo kuwafikia hata walio mikoa mengine. Soko hili limeanzishwa kuwasaidia wakulima, wafanyabiashara, wasafirishaji pamoja na watu wengine kulifikia soko la ndani na kimataifa tena kwa bei rafiki wanapouza au kununua bidhaa.

Mfumo wa Stakabadhi za Ghala

Ili kuelewa vizuri soko la bidhaa kwa mazao hapa nchini, unatakiwa kuwa na uelewa na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRS). Huu ni mfumo ambao bidhaa zinatunzwa katika maghala yaliyosajiliwa kwa ubora wa hali ya juu na kisha mhusika/aliyeweka bidhaa (mkulima, mfanyabiashara au mzalishaji) anapatiwa risiti ya ghala.

Risiti inayotolewa huanisha vitu muhimu kama umiliki, thamani, aina na ubora wa bidhaa zinazowekwa. Kwenye ghala, bidhaa hutunzwa katika mazingira yanayozingayia ubora na usalama wa hali ya juu mpaka pale mhusika anapokuwa tayari kuyachukua kwa ajili ya kufanya biashara. Baadhi ya mazao katika mfumo huu ni pamoja na kahawa, karanga mbichi, mahindi, tumbaku, mpunga, chai, alizeti na pamba.

Risiti ya ghala inaweza kuwa ya kawaida au ile ya kielektroniki na bidhaa zilizoorodheshwa hutunzwa hadi pale mhusika aliyeandikwa katika risiti atakapohitaji kuzitoa. Mfumo huu kwa kiasi kikubwa unasaidia kupiga vita vitendo vya unyonyaji hasa kwa wakulima wadogo kwani baada ya mavuno wengi wao walikuwa wakilazimika kuuza bidhaa zao kwa bei ya kutupa na kupata hasara. Mfumo huu pia unabana kuuza bidhaa bila kuzingatia ubora.

Jinsi Soko la Bidhaa Tanzania linavyofanya kazi

  1. Muuzaji/Mhusika anaweka bidhaa katika ghala ambalo limesajiliwa. Kwenye ghala, bidhaa hizo zinapimwa ubora kabla ya kukubaliwa.
  2. Mhusika/Mtoa huduma wa ghala anatoa risiti.
  3. Muuzaji/Mhusika anaweza kuamua kuchukua mkopo benki au taasisi nyingine ya fedha na kutumia risiti ya ghala kama dhamana.
  4. Muuzaji/Mhusika anaweka oda ya kuuza kwa TMX kupitia mtandao, simu ya mkononi au kwa kutembelea ofisi za TMX.
  5. TMX inatafuta mnunuaji ambaye anatakiwa kuweka fedha moja kwa moja kwenye akaunti ya benki ya muuzaji.
  6. Mnunuaji anaweka oda ya kununua na TMX kwa ajili ya bidhaa husika.
  7. Siku ya makabidhiano TMX, anayeuza na anayenunua wanafananisha oda zao na biashara inafanyika.
  8. Benki husika inafanya taratibu zinazotakiwa kuhakikisha fedha zinafika kwa muuzaji na anayenunua anapewa umiliki wa bidhaa.

Masoko mengine Afrika

Kuna masoko kadhaa ya bidhaa Afrika Mashariki. Soko la Kenya lililopo jijini Nairobi lilianzishwa mwaka 2005. Ndio la kwanza kabisa katika ukanda huu. Hivi sasa soko hilo linatoa huduma zake zote mtandaoni ambapo wanafanyabiashara wanaweza kufanya biashara kwa njia ya mtandao.

Soko la nchini Ethiopia (ECX) lilianzishwa Aprili mwaka 2008 na ni soko la kwanza Afrika kuwa na mfumo wa malipo siku moja baada ya taratibu za makabidhiano ya bidhaa kukamilika. Soko la Rwanda (EAX) lilizinduliwa Kigali mwaka 2014 na linashika nafasi ya tatu kwa ukubwa baada ya Afrika Kusini na Ethiopia.

 

IMEANDIKWA NA GIZA MDOE NA KUTAFSIRIWA NA PATRICIA RICHARD.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter