Mtandao umerahisisha uuzaji na manunuzi ya bidhaa lakini kupitia mtandao huo huo, baadhi ya watu wamekuwa wakifanya uhalifu, utapeli na udanganyifu. Ikiwa unataka kufanya manunuzi yoyote kupitia mtandao inakupasa kuwa makini ili kuepuka kutapeliwa.
Nini cha kufanya ili kuhakikisha ununuzi wako unakwenda salama?
Kuwa makini unapofanya malipo mtandaoni. Simu zinaweza kufanya kila kitu kama kompyuta lakini haimaanishi kuwa watu huweka ulinzi wa kutosha kwenye simu kama wanavyofanya kwenye kompyuta. Simu nyingi hazina vifaa na programu za kujikinga hivyo ni rahisi kwa matapeli kuvamia simu na kufanya lolote wanalotaka ikiwa ni pamoja na kuchukua fedha katika akaunti ya fedha. Hakikisha simu yako ina usalama wa kutosha.
Usitumie Wi-Fi za kijamii wakati wa kufanya malipo mtandaoni. Kila wakati unavyoingiza habari binafsi kwa kupitia Wi-Fi za umma unajiweka katika hatari ya kuibiwa utambulisho wako. Mara nyingi huduma hizi hazilindi taarifa binafsi hivyo ni rahisi kwa matapeli kupata taarifa zako muhimu na kuzitumia kufanya uhalifu.
Badilisha nywila(password) yako mara kwa mara. Sio jambo la kufurahisha kufanya mabadiliko ya nywila yako kila wakati, jambo ambalo linaweza kusababisha usahaulifu, lakini ikiwa unataka fedha zako ziwe salama katika akaunti yako ya benki unashauriwa kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ili kulinda akaunti yako.
Usibofye links (viungo) katika barua pepe. Viungo vinavyotumika kufanya utapeli huomba habari binafsi au habari kuhusu akaunti yako ili kuweza kufanya wizi. Epuka kubofya link yoyote itakayotumwa kupitia barua pepe. Ili kuhakikisha link husika ni ya salama unaweza kuwapigia simu wahusika au unaweza kutembelea tovuti ili kuhakikisha. Tovuti halisi hazitauliza habari muhimu kwa barua pepe.
Aidha, angalia sera za faragha kuhusu kampuni husika (privacy policy). Kwa kusoma sera hizo ni rahisi kujua kampuni hufanyia nini habari binafsi za watumaji wa mtandaoni. Watu wengi hupuuzia jambo hili bila kuzingatia athari zinazoweza kutokea. Hivyo ni muhimu kuwa makini na masuala haya ili kuepuka utapeli wowote unaoweza kutokea kupitia mitandao.