Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP) Lilian Liundi amesema hadi sasa, bado wanawake wanakumbwa na changamoto ya unyanyasaji wa kijinsia, akiongeza kuwa Mkoa wa Manyara unaongoza kwa vitendo hivyo. Lilian amesema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa anaongea na waandishi wa habari. Amesisitiza kuwa bado nguvu kubwa inahitajika ili kusaidia wanawake kujitambua na jamii kuachana na mila potofu.
Katika kongamano litakalofanyika Septemba 05 hadi Septemba 08 mwaka huu, TGNP watajikita katika kuelimisha wanawake na watoto wa kike ili wapate elimu na nia ya kujikwamua kiuchumi. Lilian ameongeza kuwa wamepanga kuleta wanawake maarufu ili wengine wajionee kuwa bado nafasi ya kujikwamua ipo, hali itakayopelekea wao kufanya makubwa ndani ya jamii.
Mbali na hayo, elimu ya kufanya maamuzi, uwekezaji na ujenzi wa nguvu ya pamoja itatolewa ili wanawake wapate fursa ya kujikomboa kiuchumi. Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na TGNP kwa kushirikiana na taasisi nyingine binafsi litahudhuriwa na watu takribani 1,000 kutoka mikoa mbalimbali pamoja na viongozi wa serikalini.