Home BENKI Zanzibar kutumia rasilimali mbadala ya bahari kukuza uchumi

Zanzibar kutumia rasilimali mbadala ya bahari kukuza uchumi

0 comment 123 views

Raisi wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema serikali ya awamu ya nane imeamua kufanya mapinduzi ya uchumi kwa kuendeleza uchumi wa bluu.

 

Dk Mwinyi amesema serikali inaweka mkazo katika kuziimarisha sekta za huduma ikiwemo utalii ambayo ni mhimili wa uchumi wa visiwani humo.

Raisi Mwinyi alisema hayo wakati wa hafla iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa viongozi waandamizi na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyofanyika viwanja vya Hoteli ya Verde.

 

Alisema serikali imelenga kukuza uchumi wa bluu kwa kuzitumia kikamilifu rasilimali zinazohusiana na bahari ikiwemo shughuli zinazohusu sekta ya utalii, uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi, uvuvi wa bahari kuu, ukulima wa mwani, ufugaji na usindikaji samaki pamoja na mazao mengine anuwai ya bahari.

 

Alibainisha kuwa miaka ya nyuma wananchi wengi walitegemea ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji kuendesha maisha yao ambapo kwa sasa ardhi hiyo hiyo inategemewa zaidi kwa ujenzi wa makazi, viwanda na shughuli nyingine za uchumi.

 

Kutokana na changamoto hiyo alisema serikali yake imeamua kutumia rasilimali mbadala ya bahari pamoja ma kuimarisha sekta za huduma.

 

Alimuahidi  Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kumpa timu maalumu  ya kushirikiana na benki hiyo katika kufanya kazi huku akisisitiza kuwa Serikali yake imeamua kutoa ushirikiano mzuri kwa  sekta binafsi ambapo imekusudia kwa dhati kuwa wadau wezeshi wa sekta binafsi kwa kuwawekea mifumo rafiki na mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi bila ya kikwazo.

“Nimefurahishwa sana kusikia benki imehamasika kutokana na mwelekeo wa maendeleo na dira yangu ya kuijenga Zanzibar mpya na kuamua kutuunga mkono katika jitihada zetu za kufanikisha malengo yetu tuliyoyakusudia, ahsanteni kwa moyo wenu huo wa kizalendo”,alisema.

Alisema  hamu ya benki  kushirikiana na Serikali hasa katika masuala ya uchumi wa Buluu imemtia moyo na ana imani kubwa kwamba mashirikiano hayo yataongeza kasi ya uzalishaji na sekta zinazotegemea mazao ya baharini kama vile viwanda na usindikizaji vitaibuka na kuimarika.

Alisema dhamira ya Serikali  ni kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji ambapo pia, Serikali imejipanga kuendeleza utalii, kukuza biashara na viwanda na kushajiisha uwekezaji katika maeneo mapya ya uchumi.

Aliitaka kuwa na ujasiri wa kuwapatia mikopo wananchi wanaojishughulisha katika sekta ya kilimo, uvuvi wa kawaida, ujasiriamali na ufugaji, wauzaji wa biashara ndogo ndogo na za kati  wanahitaji kuwezeshwa zaidi ili biashara zao ziwaletee kipato chenye tija itakayoweza kuwakwamua na umasikini.

Nsekela akiwasilisha mada juu ya shughuli za benki hiyo na jinsi ilivyojipanga katika kushirikiana na Serikali na kueleza iko tayari na kumuomba Rais aipe timu kwa ajili ya kufanya kaziili kuleta maendeleo ya kasi na chanya.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter