Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Ummy Mwalimu, amelitaka baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamaizi wa Mazingira (NEMC) lisiwe kikwazo kwa wawekezaji nchini.
Waziri Ummy alisema uchumi wa viwanda utafikiwa kwa kuweka mazingira mazuri yatakayovutia wawekezaji.
Akizungumza na Menejimenti ya NEMC jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy aliwataka pia kuimarisha ofisi zao za kanda na kuwajengea uwezo wafanyakazi wake ili wamudu kasi ya uwekezaji na kuondoa mrundikano wa mambo katika ofisi za makao makuu.
Alilitaka baraza hilo kuwashauri wawekezaji huku akisema baadhi ya wataalamu elekezi sio waaminifu kwa kuwa wamekuwa wakirefusha mchakato wa upatikanaji wa huduma kwa wawekezaji zikiwemo za utoaji wa vibali jambo linaloitia NEMC doa.