Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imetenga dola za Kimarekani milioni 15 kuunga mkono sekta zilizochini ya Uchumi wa Buluu.
Hayo yamebainishwa wakati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akiupokea ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, ukiongozwa na Rais wake Dk. Akinwumi Adesina Ikulu, Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kuunga mkono miradi mbalimbali ya Maendeleo Zanzibar ikiwemo ya kijamii katika sekta ya afya , barabara, maji na sekta ya usafiri.
Dk. Mwinyi ameitumia fursa hiyo kuueleza ujumbe huo wa AfDB juu ya hatua zinazoendelea na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kusimamia sekta zilizo chini ya uchumi wa buluu ambapo kwa upande wa utalii amewaeleza unachangia asilimia 30 ya pato la nchi.
Rais huyo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Dk. Adesina alimuelezea mwenyeji wake Rais Dk. Mwinyi miradi ambayo Benki hiyo inasaidia zaidi kuwa ni ujenzi wa barabara na sekta nzima ya usafiri.
Amesema kwa sasa Benki yake inasaidia ujenzi unaoendelea wa barabara ya Bububu-Mahonda-Mkototoni, ujenzi wa barabara Tunguu-Makunduchi na ya Mkoani- ChakeChake.
Vilevile benki hiyo imejikita kusaidia ujenzi wa uwanja wa ndege mpya wa Pemba na miradi kadha ikiwemo ya maji na ujenzi wa masoko.