Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIBIASHARA Wadau mitandao ya kijamii waombwa kuelimisha umuhimu wa kulipa kodi

Wadau mitandao ya kijamii waombwa kuelimisha umuhimu wa kulipa kodi

0 comment 204 views

Wadau wa Mitandao ya Kijamii wameaswa kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha jamii umuhimu wa kulipa kodi na kudai risiti halali.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Fedha Benny Mwaipaja ametoa wito huo wakati akifungua Kongamano la wadau wa mitandao ya Kijamii na Wizara ya Fedha Mkoani Morogoro unaofanyika Oktoba 23 hadi 24, 2023.

Amesema kuwa mitandao ya kijamii imekuwa njia ya kigitali ya kuifikia jamii kwa haraka na kwa ukubwa na amewaomba wadau hao kutumia jukwaa hilo kuielimisha jamii umuhimu wa kulipa kodi ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi na kuleta maendeleo kwa wananchi.

Amewata wanunuzi kudai risiti zinazolingana na kiasi cha fedha walichotoa kila wanapofanya manunuzi na wauzaji kutoa risiti wanapouza bidhaa na huduma mbalimbali.

“Wizara inawatambua nyie ni wadau muhimu sana naomba mkawe vinara wa kuelimisha jamii ili kuongeza elimu ya masuala ya kodi na kuelezea kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kusimamia uchumi na pia kuwaelimisha jamii kuhusu agenda ya maendeleo ya taifa na miradi inayotekelezwa na serikali kwa ajili ya maslahi ya watanzania ikiwemo miradi ya kimkakati,” amesema Mwaipaja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kongamano hilo, Mathias Canal ameipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa kongamano hilo na kusema kuwa hiyo ni fursa ya kurahisisha utendaji kazi wao kwa umma haswa kwa kujengewa uwezo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Wizara hiyo.

Canal ameongeza kuwa, Wizara hiyo iendelee kuhakikisha inatoa ufafanuzi kwa umma kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali na umuhimu wa mikopo ili kuondoa sintofahamu kwa jamii kuhusu mikopo ya serikali.
Kongamano hilo la Siku mbili linatoa fursa kwa wadau wa mitandao ya kijamii kujifunza masuala mbalimbali kuhusu Wizara hiyo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter