Home VIWANDANISHATI EWURA yatangaza bei mpya za mafuta

EWURA yatangaza bei mpya za mafuta

0 comment 136 views
Na Mwandishi wetu

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo hii imetangaza bei mpya ya bidhaa za mafuta ya petrol pamoja na mafuta ya taa ambapo kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Godwin Samwel bei za rejareja za petrol zimeongezeka kwa Sh. 10 kwa lita, ongezeko la asilimia 0.53 huku bei za mafuta ya taa zikipungua kwa Sh. 19 kwa lita moja ambayo ni sawa na asilimia 1.04.

Kaimu Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa ongezeko katika mafuta ya petrol na dizeli limetokana na ongezeko la bei ya bidhaa hizo katika soko la dunia pamoja na gharama za juu za usafirishaji, kitendo ambacho kimeathiri masoko ya ndani moja kwa moja. Ameongeza kuwa punguzo katika mafuta ya taa inatokana na kupungua kwa gharama za usafirishaji japokuwa bidhaa hiyo nayo imepanda bei katika soko la dunia.

Samwel ametaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana kwa urahisi. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dk, Benson Bana ambaye ni mtaalamu katika masuala ya uchumi hapa nchini amesema kupungua kwa bei ya mafuta ya taa ni jambo la faraja kwa watumiaji wa hali ya chini kwani kuanzia sasa watapata unafuu pale watakapohitaji bidhaa hiyo.

Kuhusu ongezeko la bei ya petrol na dizeli, Dk.Bana amesema EWURA hupandisha na kushusha bei kulingana na hali ya soko la dunia akiongeza kuwa ongezeko hilo ni pigo kwa watumiaji lakini ni faida kwa wafanyabiashara huku akidai ongezeko hilo linaweza kupelekea gharama za usafiri kupanda.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter