Home BENKI Msichimbie fedha ndani: Waziri Dkt Nchemba

Msichimbie fedha ndani: Waziri Dkt Nchemba

0 comment 320 views

Watanzania wametakiwa kutumia benki kuhifadhi fedha zao ili kuhakikisha usalama wa fedha hizo na usalama wao na kuacha tabia ya kuhifadhi fedha majumbani.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema hayo jijini Dodoma wakati akizundua Tawi la Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Nchemba amesema ni vema wananchi wakajenga utamaduni wa kutumia benki kwa kuwa uendeshaji wa uchumi wa kisasa unategemea zaidi matumizi ya utaratibu wa kibenki ambao kwa sasa umerahisishwa na unapatikana kwa urahisi.

“Utaratibu wa kuchimbia fedha ni utataribu wa kizamani, benki sasa zipo kiganjani kwanini uchimbie fedha?. Popote ulipo unawezakupata huduma za benki”, amesisitiza Dkt Nchemba.

Dkt. Nchemba amebainisha kuwa sema Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na benki zote hapa nchini kama utekelezaji wa sera jumuishi za masuala ya kifedha na kiuchumi zinazolenga kuwasogezea wananchi huduma za kifedha karibu.

‘’Naomba kutumia fursa hii kuwaomba wafanyabiashara, watumishi wa umma na binafsi, viongozi wa Serikali wa ngazi mbalimbali na wananchi kwa ujumla kuiunga mkono na kuitumia Benki ya PBZ katika shughuli zetu za kiuchumi, kwani benki hii imekuwa ikitoa huduma zake kwa uaminifu mkubwa na kwa riba nafuu.’’

Akitoa salamu za Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Zanzibar, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Ali Suleiman Amir amesema Serikali imeamua kuhakikisha huduma za fedha zinawafikia wananchi wote kwa urahisi.

Ameipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kutimiza azma ya Serikali kwa kufungua matawi yao katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya PBZ, Dkt. Muhsin Salim Masoud, ameeleza kuwa Benki hiyo ina vituo vya kutolea huduma takribani 45 ambapo vituo 34 vipo Zanzibar na vituo 11 vikiwa Tanzania Bara huku akiahidi kuongeza vituo vya kutolea huduma ili kuwafikia watanzania wengi zaidi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter