Home KILIMOKILIMO BIASHARA Rais Dkt. Samia atoa maelekezo bei ya mahindi vijijini na mjini

Rais Dkt. Samia atoa maelekezo bei ya mahindi vijijini na mjini

0 comment 198 views

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua mahindi ya wakulima kwa Sh. 600 kwa kilo kwa vijijini na Sh. 650 kwa mjini.

Rais Samia amesema hayo Julai 16, 2024 wakati akizindua vihenge na maghala ya kisasa ya katika eneo la Kanondo, Mkoani Rukwa.

Wakati wa mazungumzo yake na wananchi wa Mkoa wa Rukwa, Rais Dkt . Samia ameelekeza kuwa mbolea za ruzuku ziendelee kuwepo na kusisitiza mahindi yanunuliwe kutoka kwa wakulima wa vijijini kwa gharama ya shilingi 600 kwa kilo, na mjini shilingi 650 kwa kilo.

Rais Samia ambae alimpa nafasi ya kasalimia wananchi Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambapo wakati wa salamu zake alimkatisha na kusema “Waziri kabla hujaendelea hapo kwenye malipo, unakumbuka nilikupa agizo baada ya kilio cha Mkoa kwamba mahindi sasa vijijini ununue kwa Shilingi ngapi? 600 sawa kwa vijijini na mjini 650, haya endelea,” alisema Rais Dkt. Samia na kushangiliwa na wananchi.

Aidha, alitilia mkazo kwa wananchi kutosafirisha mahindi nje ya nchi bila vibali vya Wizara ya Kilimo, na taratibu nyingine zinazotakiwa kwa kuwa zinaathiri uchumi na soko la kibiashara.

Kuhusu mizani ya kidigitali, Rais Dkt. Samia alielekeza ziongezwe kwa wingi katika vituo vya Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) ili kurahisisha huduma kwa wakulima kwa kupata haki stahiki ya uzito wa mazao yao.

Katika salamu zake, Waziri Bashe ameeleza uwepo wa mashine za kidigitali katika vituo vya manunuzi utarahisisha zoezi la upimaji na malipo ya wakulima.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akizungumza mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Ucheleweshwaji wa malipo kama mliokutana nao mwaka jana hautokuwepo, sasa hivi malipo hayatazidi siku saba mpaka 14 utakuwa umepata fedha yako katika akaunti yako na hilo tatizo litakuwa limekwisha,” ameahidi Waziri Bashe.

Mradi huo utaiwezesha NFRA kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka za aina tofauti kama vile mahindi, mtama na mpunga katika Mkoa wa Rukwa kutoka tani 33,500 hadi tani 58,500, kwa maana ya ongezeko la vihenge tani 20,000 na maghala tani 5,000.

Maghala hayo ya kisasa yana mfumo mzuri wa kupitisha hewa ambao pia unaoruhusu ufanisi katika uhudumiaji mazao (improved ventilation sytem and improved logistical system); ikiwa ni pamoja na utumiaji wa zana mbalimbali za kazi (matrekta, mizani, elevators).

Mradi huo ulianza mwezi Julai 2019 na umegharimu Dola za Marekani milioni 6,019,000 sawa na takribani shilingi bilioni 14.

NFRA inaendelea kujipanga kuongeza uwezo wa teknolojia ya vihenge na maghala ili kuendana na uzalishaji wa chakula hapa nchini.

Viongozi mbalimbali walishiriki katika uzinduzi huo, akiwemo Hussein Bashe Waziri wa Kilimo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Dkt. Andrew Kolimba Bodi na Menejimenti ya NFRA.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter