Home VIWANDAMIUNDOMBINU Tanzania kununua helikopta kuchunguza madini ardhini

Tanzania kununua helikopta kuchunguza madini ardhini

0 comment 196 views

Serikali ya Tanzania imesema ina mpango wa kununua helikopta itakayofungwa vifaa maalum vya uchunguzi wa madini ardhini.

“Tutakwenda kununua helkopta ambayo tutaifunga vifaa vya utafiti kwa ajili ya ‘kuscan’ ardhi yetu kuweza kufahamu chini ya ardhi kuna nini,” ameeleza Waziri wa Madini Antony Mavunde.

Waziri Mavunde anaeleza “bahati nzuri hivi sasa katika Dunia ya leo vifaa hivi vinaweza kwenda chini ya ardhi kuanzia mita 500 hadi kilomita moja kuweza kubaini miamba yenye viashiria vya madini, ili baadae tuweze kufanya uchorongaji, na tuweze kujua tuna madini kiasi gani chini ya ardhi.”

Waziri Mavunde ameeleza hayo Oktoba 15, 2024 kupitia mjadala uliofanyika kwa njia ya mtandao wa kueleze mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita katika uboreshaji wa sekta ya madini nchini.

Aidha, Waziri Mavunde akizungumza jijini Dodoma ameeleza kuhusu mikakati iliyopo ndani ya wizara kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025.

Ameeleza kuwa katika kuimarisha uchimbaji wenye tija na uhakika serikali itajenga maabara ya kisasa mkoani Dodoma na Geita ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupeleka sampuli zao kwa uchunguzi.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa , wizara itaendelea kutumia mpango wa ushirikiano baina ya taasisi za Umma na taasisi za sekta binafsi katika kuendeleza miundombinu ya barabara na nishati ya umeme sehemu zenye uchimbaji.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa madini Dkt. Steven Kiruswa ameeleza kuwa, elimu kuhusu tozo zinazotozwa, wajibu wa mmiliki wa leseni kwa jamii , ushiriki wa Watanzania katika uvunaji wa rasilimali madini na utunzaji mazingira katika shughuli za uchimbaji ilitolewa kwa wachimbaji wadogo katika Kamati za Maendeleo za Kata.

Awali , akiwalisha taarifa kuhusu mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwasogezea huduma za Ugani katika mkoa wa Dodoma kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini , Kamishna wa Madini Dkt. AbdulhRaman Mwanga amesema Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya zebaki katika wilaya ya Chamwino na Bahi.

Sambamba na hapo Dkt. Mwanga amesema Wizara itaendelea kuboresha mifumo ya utoaji na usimamizi wa leseni za madini pamoja na kuwezesha utafutaji wa madini kwa njia ya uchorongaji.
Mikakati mingine ni pamoja na kutoa elimu kuhusu athari za mazingira zitokanazo na uchimbaji wa madini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter