Home FEDHA Wananchi Mbeya wachekelea elimu ya fedha

Wananchi Mbeya wachekelea elimu ya fedha

0 comment 92 views

Wakazi wa Jiji la Mbeya wameipongeza Serikali kwa kuwasogezea elimu ya fedha na huduma mbalimbali za fedha karibu nao.

Wametoa pongezi hizo katika Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.

Wamesema elimu wanayoendelea kuipata katika maadhimisho hayo ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wao binafsi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Baadhi ya wananchi wakipata elimu ya fedha katika Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.

Rehema Kassiba wa Kumekucha Saccos ni miongoni mwa wananchi hao, anasema maadhimisho hayo yamewarahisishia upatikanaji wa elimu na huduma za fedha kwa kuwa Serikali imezisogeza huduma muhimu za masuala ya fedha katika maadhimisho hayo.

Ameipongeza Serikali kwa kuandaa maadhimisho hayo na kuahidi atakuwa balozi mzuri kwa kuifikisha elimu aliyoipata kwa wananchi wengine ambao hawajapata nafasi ya kufika viwanjani bua Nzowe yanapofanyika maadhimisho hayo.

“Elimu hii ni nzuri na muhimu kwetu lakini tunaiomba Serikali iandae utaratibu wa kufikisha elimu hii katika maeneo ya vijijini kwa kuwa muda wa maadhimisho haya ni mchache sio rahisi kwa wananchi wote kuhudhuria hususan wale wanaotoka vijijini”, amesema Kassiba.

Naye John Mwakipasile, mjasiriamali wa soko la Mwanjelwa amesema maadhimisho hayo yamewaongezea uelewa wa fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Fedha.

Amesema katika maadhimisho hayo wamepta ujuzi wa matumizi sahihi ya huduma za fedha katika kukuza biashara zao, utamaduni wa kujiwekea akiba, kukopa na kulipa madeni.

Kwa upande wao, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Mbeya, nao wameishikuru Serikali kwa kupeleka Maadhimisho hayo jijini hapo kwa kuwa yamewawezesha kuwapata wananchi wengi ndani ya muda mfupi.

Mratibu wa Mikopo wa Jiji la Mbeya, Aksa Njidile ni miongoni mwa Maafisa hao, ambaye aliwakaribisha wananchi kwa kutembela maadhimisho hayo ili wapate elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa.

Amesema wakitembelea katika maadhimisho hayo pamoja na mambo mengine, watapata elimu ya mikopo mbalimbalimbali inayotolewa na Serikali hususan ile ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.

Wanafunzi wakipata elimu ya fedha katika Maadhimisho ya Nne ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayoendelea katika Viwanja vya Ruanda-Nzovwe, jijini Mbeya.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter