Home FEDHAMIKOPO BoT yafungia wakopeshaji 69

BoT yafungia wakopeshaji 69

0 comment 38 views

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefungia  jumla ya majukwaa na programu tumizi “applications” 69 zinazojihusisha na utoaji wa mikopo kidigitali.

Taarifa ya BoT iliyosainiwa na Gavana Emmanuel Tutuba Novemba 21, 2024 inaeleza kuwa majukwaa na programu hizo zimeshindwa kukidhi matakwa ya Mwogozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidigitali wa mwaka 2024 uliotolewa na Benki Kuu Agosti 27, 2024 (Guidance Note on Digital Lenders Under Tier 2 Microfinance Service Providers, 2024).

Taarifa hiyo inaeleza kuwa mwongozo huo unalenga kuimarisha usimamizi wa Watoa HUduma Ndogo za Fedha Daraja la Pili nchini na kuhakikisha uzingatiwaji wa Kanuni za Kumlinda Mlaji wa Huduma za Fedha ikijumuisha uwazi, uwekaji wa tozo na riba, njia za ukusanyaji wa madeni na utunzaji wa taarifa binafsi za wateja na kulinda faragha zao.

BoT imeeleza kutoa huduma ya mkopo kwa njia ya mtandao bila leseni ni uhalifu.

BoT, imewataka Watoa Huduma za Mikopo Mitandaoni kuzingatia sheria na miongozo mbalimbali katika utoaji wa huduma hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina na wahariri wa vyombo vya habari nchini wiki iliyopita, Kaimu Meneja Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Dickson Gama amesema Benki Kuu kwa kushirikiana na taaasisi zingine zimechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha watoa huduma hao wanafuata sheria zilizowekwa.

“Tunashirikiana na TCRA kuwafungia na kuwaondoa kwenye mtandao wanaofanya biashara hiyo bila leseni, lengo ni kuhakikisha kwamba kila anayetoa mikopo mitandaoni afuate sheria na taratibu zilizowekwa. Anayetoa mikopo mtandaoni pasipokuwa na leseni ni mhalifu,” amesisitiza Gama.

Naye, Meneja Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Huduma Ndogo za Fedha, Mary Ngassa, ameeleza kuwa kufuatia changamoto ya ukiukwaji wa sheria katika utoaji wa mikopo kidijitali, Benki Kuu ilitoa ‘Mwongozo kwa Watoa Huduma Ndogo za Fedha wa Daraja la Pili wanaotoa huduma za mikopo kwa njia ya kidijitali wa mwaka 2024’, mwezi Agosti 2024, ambapo Kifungu Na. 3.0 cha Mwongozo huo kimewataka watoa mikopo hao pamoja na mengine kuwa na leseni na kutunza faragha za wateja wao.

Amebainisha kuwa ili mtoa huduma ndogo za fedha kuruhusiwa kutoa mikopo kidijitali anatakiwa kuwa na leseni ya kuendesha biashara ya Huduma Ndogo za Fedha chini ya Daraja la 2 chini ya kifungu Na. 16 cha Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 na awe amefuata matakwa ya Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act) ya mwaka 2022 na kanuni zake.

Kuhusu udhalilishaji wa wakopaji mtandaoni Meneja msaidizi huyo amesema, “utaratibu ni kwamba mtu amekopa, hajalipa anapaswa notisi ya siku 14, hajajibu anapewa siku 7 na baada ya hapo unachukua hatua kwa utaratibu kwa kuchukua dhamana yake kwa njia ya kisheria, lakini wanapotishia watu na kuwadhalilisha ni kinyume na sheria na mteja unaweza kumshitaki.”

 

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter