Home FEDHAMIKOPO Wakopeshaji waelezwa umuhimu wa taarifa za mikopo

Wakopeshaji waelezwa umuhimu wa taarifa za mikopo

0 comment 32 views

Watoa huduma ndogo za fedha wameelezwa umuhimu wa kujiunga katika mfumo wa taarifa za mikopo ili kuboresha uwezo wa watoa huduma hao katika kufanya tathmini ya mikopo kwa usahihi na kupunguza mikopo chechefu.

Wataalam kutoka kampuni za kuchakata taarifa za mikopo za Dun & Bradstreet na Credit Info, wameeleza hayo

Wakati wakiwasilisha mada kwa nyakati tofauti katika semina kwa washiriki kutoka kampuni za huduma ndogo za fedha Kanda ya Kusini, inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Mtwara.

Akizungumza katika semina hiyo iliyoandaliwa na BoT, Afisa Maendeleo ya Biashara wa Dun & Bradstreet Tanzania, Brian Magai, amesema ni wajibu wao kusaidia taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha na vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) kuuelewa vizuri mfumo wa taarifa za mikopo, kushiriki na kutoa taarifa hizo kila wanapotaka kutoa mikopo.

“Faida zinazotokana na kutumia taarifa za mikopo kwa wakopeshaji ni pamoja na kudhibiti mikopo chechefu, kupunguza hasara na kuongeza mapato,” amesema.

Naye, Meneja Msaidizi wa Credit Info kwa upande wa taasisi ndogo za fedha, Emmanuel Matee, amezikumbusha kampuni zinazotoa huduma ndogo za fedha kwamba wana wajibu wa kutumia huduma zitolewazo na taasisi zao zinazochakata taarifa za mikopo ili waweze kuimarisha shughuli zao.

Pamoja na maelezo yao, wataalamu hao kutoka kampuni hizo, walitoa mifano mbalimbali hai ya namna ya kutumia taarifa za mikopo, ikiwemo namna ya kutuma taarifa kwa kampuni hizo, pamoja na kuomba taarifa za wakopaji wanaohitaji mikopo kutoka kwao.

Aidha, wataalamu hao wameishukuru BoT kwa kuwaandalia fursa ya kukutana na wadau wao muhimu katika maendeleo ya sekta ya fedha nchini.

Nao washiriki wa semina hiyo, wengi wakiwa kutoka Wilaya zilizoko katika mikoa ya Mtwara na Lindi, wameipongeza BoT  na kusema elimu hiyo itawasaidia katika shughuli zao kwa kuhakikisha wanatumia taarifa hizo.

Benki Kuu imeandaa mfululizo wa semina kwa wadau mbalimbali wa sekta ya fedha kutoka Kanda ya Kusini, kuanzia Desemba 02 hadi 06 2024, ili kuwajengea uelewa kuhusu mfumo wa taarifa za mikopo.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter