Takribani asilimia 70 ya bajeti ya serikali ya Tanzania inatumika katika sekta ya Ununuzi na Ugavi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, amesema hayo wakati akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la 15 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi nchini linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha.
Dkt. Biteko amewataka wataalamu wa Ununuzi na Ugavi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia kada ya Ununuzi na Ugavi nchini.
“Sekta ya Ununuzi na Ugavi ndio eneo pekee linalochukua takribani asilimia 70 ya Bajeti ya Serikali, hivyo uadilifu pekee ndio utakaosaidia fedha kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa hasa katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema Dkt. Biteko.
Amewataka wataalamu hao kuzitendea haki taaluma zao kwa kufanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha sekta ya ununuzi na ugavi inawatoa watu kwenye umasikini.
Aidha, Dkt. Biteko aliwaasa wataalamu hao kuzingatia na kuyaishi yale yaliyopo kwenye sheria za manunuzi kwa kufanya kazi yenye tija, uwazi na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwenye masuala yote ya manunuzi ya Umma.
‘’Serikali iliamua kuanzisha sheria ya manunuzi ili kuwa na manunuzi yenye tija, kupata bidhaa zenye ubora na wakati, na kuondoa mianya ya rushwa, hivyo naomba mkutano huu uzingatie yale yanayotafsiriwa kwenye sheria hiyo’’ alisema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko aliipongeza Bodi ya Usimamizi wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), kwa hatua mbalimbali inazochukua hasa kwa wale wanaoenda kinyume na maadili ya sekta hiyo na kusisitiza kuwa Serikali kupitia bodi hiyo haitasita kuwachukulia hatua kali watumishi ambao watashindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Hata hivyo, Dkt. Biteko amewataka washiriki wa Kongamano hilo kujifanyia tathimini kuhusu utendaji wao wa kazi ili kuondokana na Changamoto zinazoweza kuichafua taaluma ya ununuzi na ugavi.
“ Zipo sauti nanyi mnazisikia, ili uweze kupata tenda lazima kuwa na urafiki na Afisa ununuzi, wanasema ukifuata taratibu za ununuzi gharama zinaongezeka zaidi ya kawaida, wengine wanasema siri za tenda zinapatikana miongoni mwa watumishi, wengine wanalaumu na wengine wanasifia, Jambo la msingi sikilizeni sauti za watu na mjitathimini,” amesisitiza Dkt. Biteko
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande.Awali akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande alisema kuwa Wizara ya Fedha imeendelea kuwapa thamani na kutoa kipaumbele kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika eneo lao la kazi ili kukuza uchumi.