Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIFEDHA Wadau waipa Tanzania Dola za Marekani bilioni 2.7

Wadau waipa Tanzania Dola za Marekani bilioni 2.7

0 comment 243 views

Takribani Dola za Marekani bilioni 2.7 zimetolewa na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kuisaidia Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kati ya fedha hizo, asilimia 51 ni misaada na asilimia 49 ni mikopo yenye masharti nafuu.

Hayo yameeleza na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, David Concar katika mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo ngazi ya Juu ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Mkutano.

Balozi Concar amesema kuwa wadau wa maendeleo wanampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoyafanya na wanayaona mabadiliko mbalimbali anayofanya katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, biashara pamoja na uwekezaji katika sekta ya uzalishaji.

Ameeleza kuwa wadau wa maendeleo wako tayari kuendelea kuiwezesha nchi kufikia maendeleo ya kukuza uchumi wa wananchi.

Akifungua mkutano huo, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia imedhamiria kuwa na maendeleo endelevu ambayo hayamuachi Mtanzania yoyote nyuma kwa kufanya uwekezaji katika Sekta za Uzalishaji.

“Kipaumbele kimewekwa kwenye uwekezaji katika mtaji wa binadamu, maendeleo ya miundombinu, kuhamasisha ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii, utawala bora, kuwawezesha wanawake na uhifadhi wa mazingira,” ameeleza Dkt. Nchemba.

Amesema kwa kutekeleza mikakati hiyo pamoja na kukuza ushirikiano na sekta binafsi, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, Tanzania inaweza kupiga hatua kubwa kuelekea kufikia ukuaji wa Uchumi endelevu.

Dkt. Nchemba aamebainisha kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha mazingira ya ukuaji wa biashara, kuongeza ushindani na kukuza ubunifu ili kukuza uchumi wa nchi.

Aidha, amesema Tanzania pia inatumia Diplomasia ya Kiuchumi kama mkakati muhimu wa kuendeleza uchumi wake na kubainisha kuwa nchi ina dhamira kubwa ya kufuata kanuni za ushirikiano wa kimataifa wenye manufaa kwa pande zote.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter