Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Tuzo za utalii, uhifadhi Tanzania kuzinduliwa kesho

Tuzo za utalii, uhifadhi Tanzania kuzinduliwa kesho

0 comment 52 views

Tuzo za kwanza Kitaifa za Utalii na Uhifadhi nchini Tanzania zinatarajiwa kuzinduliwa kesho (Desemba 20, 2024).

Katika tuzo hizo, viongozi na watu mashuhuri wenye mchango katika sekta ya Utalii watatuzwa mwaka huu na baadaye kila mwaka.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha Desemba 18, 2024, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema licha ya uzinduzi, tuzo chache za heshima na shukrani zitatolewa ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mvumbuzi wa fuvu la mwanadamu wa kale (Zinjanthropus Boisie), Dkt. Louis Leakey na mkewe Mary Leakey ambaye baadaye yeye na watafiti wenzake walivumbua pia nyayo za binadamu wa kale aliyetembea akiwa wima (Laitori) watakuwa miongoni mwa watakaopewa Tuzo za heshima.

“Tutazindua na tuzo 11 za heshima na shukrani na ya kwanza itaenda kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mwanamaono mkuu ambaye mchango wake kupitia filamu ya Royal Tour na baadaye Amazing Tanzania.

“Dkt. Leakey na familia yake watatuzwa pia kama moja ya kutambua watu ambao matendo yao, ubunifu na tafiti zao zimetuzalishia vivutio muhimu vya utalii wetu wa sasa. Leo kwa mwaka pale Olduvai wanafika wastani wa watalii 20,000 hawa leo hawako hai lakini kazi ya mikono yao inaendelea kuleta matokeo chanya.

Hivi ndivyo namna tutakavyotambua wadau wengi zaidi kila mwaka kuenzi mchango wao,” alisema Dkt. Abbasi.

Katika tukio hilo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa akisindikizwa na Waziri wa Sekta, Dkt. Pindi Chana na Naibu Waziri Dunstan Kitandula, Mawaziri, wakuu wa Mikoa, makatibu wakuu na wadau wa utalii ndani na nje ya nchi.

Aidha, kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii kama kundi la Weusi, Frida Amani, Sholo Mwamba na vikundi kutoka mataifa ya India na China kuupamba usiku huo.

Tuzo hizo zitakuwa zikitolewa kila mwaka kuenzi mchango wa wadau wa ndani na nje ya nchi katika sekta hizo zinazoongoza kwa sasa nchini kuliletea Taifa fedha za kigeni.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter