Baadhi ya mila, desturi, imani na mfumo dume vimetajwa kuwa moja ya vikwazo vinavyowazuia wanawake na vijana wengi kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi wa jamii.
Utafiti uliofanywa na Shirika la Mazingira na Haki za Binadamu na Jinsia (Envirocare), umeonesha baadhi ya changamoto hizo zikiwemo pia rushwa ya ngono na ukosefu wa fedha kwa kundi hilo.
Msimamizi wa Mradi wa Kuwezesha Wanawake na Vijana kushiriki katika Uongozi katika mkoa wa Dar es Salaam Godlisten Muro ameeleza hayo katika semina na waandishi wa habari iliyofanyika kwa siku mbili, Machi 4-5.
“Hili ni jambo ambalo tunapaswa kushirikiana kwa nguvu zote kulipatia suluhisho.
Katika miaka ya hivi karibuni, bado tumeshuhudia changamoto nyingi zinazoikumba jamii yetu katika suala la usawa wa kijinsia na ushiriki wa makundi maalum katika uongozi.
Kupitia warsha hii, tunatarajia kuwa waandishi wa habari mtapata maarifa zaidi kuhusu changamoto na fursa zilizopo kwa wanawake na vijana katika uongozi,” amesema Muro.
Mradi huo unaotekelezwa kwa miezi 21 ulianza Disemba 2024 katika Wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni kwa ufadhili wa dola za Kimarekani 74,000 kutoka Canada.
Muro amesema “tutaangazia pia mbinu mbalimbali za kuandika na kuripoti habari zinazohusiana na ushiriki wa wanawake na vijana katika siasa na uongozi kwa njia inayojenga jamii na kuhamasisha mabadiliko chanya.
Mradi huu wa miezi 21(Disemba 2024 hadi Agosti 2026) ni muendelezo wa mradi wa awali ambao ulitekelezwa kwa takribani miezi 18 na kumalizika mwezi wa 10 mwaka 2024.
Mradi huu ulifanikiwa kufikia moja kwa moja (direct) jumla ya wanawake na vijana mia tano (500), mia moja (100) kati yao wakiwa ni wanaume na mia nne (400) ni wanawake.
Aidha idadi ya watu waliyofikiwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja ni elfu moja (1000).
Katika awamu hii ya mradi, tunatarajia kufikia wanawake 400 na vijana 300 (wanaume 150 na wanawake 150) katika mkoa wa Dar es Salaam ambao wanakabiliwa na changamoto za kushiriki katika mifumo ya utawala na vyombo vya maamuzi.
Aidha, mradi huu utawalenga kwa njia isiyo ya moja kwa moja wadau mbalimbali, wakiwemo serikali, viongozi wa kisiasa, mashirika ya kiraia, viongozi wa kidini, sekta binafsi, na vyombo vya habari, ambao wana mchango katika kuunda mazingira wezeshi kwa ushiriki wa raia wote katika michakato ya utawala na maamuzi.
Ameeleza kuwa kwa ujumla, mradi unatarajia kufikia takribani watu 30,000 kwa njia isiyo ya moja kwa moja kupitia juhudi za uhamasishaji na ushirikiano na wadau husika.
“Tunatambua kuwa waandishi wa habari mnayo nafasi muhimu sana katika jamii. Ninyi ni nguzo kuu ya kuhakikisha kuwa masuala ya kijamii, hususan ushiriki wa wanawake na vijana katika uongozi, yanajadiliwa kwa kina na kwa uwazi.
Kupitia kalamu zenu na vyombo vyenu vya habari, mnaweza kubadili mtazamo wa jamii kuhusu uongozi shirikishi na kuhakikisha kuwa wanawake na vijana wanapewa nafasi stahiki katika maamuzi ya kitaifa na kijamii,” amesisitiza Muro.
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Envirocare imeeleza kuwa licha ya hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa kuna usawa wa kijinsia katika uongozi, bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
“Ni jukumu letu sote, hususan ninyi waandishi wa habari, kuendeleza ajenda hii kwa kuhakikisha kuwa mnatoa taarifa sahihi, zenye ushawishi na zinazoweza kuleta mabadiliko.
Nawahimiza kushiriki kikamilifu katika majadiliano na kubadilishana uzoefu ili kuhakikisha kuwa tunapata njia bora za kushirikiana katika kufanikisha lengo hili,” imeeleza taarifa hiyo.