Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango anatarajia kuwasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019 leo bungeni Dodoma ikiwa ni bajeti ya tatu chini ya utawala wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli. Baadhi ya wabunge wameeleza matarajio yao na kusema kuwa wanategemea bajeti hiyo itazingatia maisha ya wananchi wa kawaida na kupunguza ada, kodi na tozo mbalimbali zilizopo hivi sasa.
Akitoa maoni yake, Mbunge wa Rufiji kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mohamed Mchengerwa amesema kupitia bajeti hiyo, serikali inapaswa kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa wananchi na kuelekeza nguvu zaidi katika kuboresha mazingira ya miundombinu ya umeme. Kwa upande wake, Mbunge wa Vinjo kwa tiketi ya chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia amesema watanzania walio wengi wamekata tamaa na wanapaswa kupewa matumaini ya kuishi kwani wanalia na hali ngumu ya maisha. Ameongeza kuwa, anatarajia bajeti hiyo itakuwa mwanga wa matumaini hasa kwa walipakodi na itaonyesha maendeleo ya watu na sio vitu.
Naye Hussein Bashe, Mbunge wa CCM Nzega Mjini amesema serikali imekuwa ikibana matumizi na kukusanya kodi kwa takribani miaka miwili sasa hivyo anatarajia bajeti itakayosomwa itachochea uzalishaji na sio kuangazia masuala ya kodi pekee.