Serikali ndio chombo kikuu kinachosimamia shughuli zote za uzalishaji kote duniani. Kukua na kuporomoka kwa uchumi kunategemea moja kwa moja mfumo wa serikali katika utendaji na usimamizi wa shughuli za kiuchumi na biashara kwa ujumla.Shughuli hizo ni pamoja na viwanda, kilimo, uvuvi, madini, usafirishaji, utalii na nyinginezo.
Ni muhimu kufahamu majukumu ya serikali katika suala zima la uendeshaji wa biashara na jinsi serikali inavyochangia katika kuleta maendeleo ya nchi. Baadhi ya majukumu ni haya yafuatayo:
Kutoa vibali vya biashara – Kupitia Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) serikali imekuwa ikitoa TIN Number inayompa mtu uhalali wa kufanya biashara. Umuhimu wa TIN Number ni kwamba mfanyabiashara ana wezowa kufanya biashara nchini na nje ya mipaka ya Tanzania. TIN hutolewa bure baada ya TRA kujiridhisha na biashara yako Soma Zaidi
Kuhakikisha Utekelezaji wa Mikataba – Serikali kupitia mahakama imekuwa ikisimamia mikataba mbalimbali inayoambatana na utiaji saini kuonyesha makubaliano baina ya pande mbili zinazokubaliana katika kuendesha biashara, ikiwa ni pamoja na mikataba ya mauzo, hisa, uwekezaji n.k
Ujenzi na uboreshaji wa Miundombinu – Serikali imekuwa ikitekeleza ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ili kuimarisha shughuli za usafirishaji na uchukuzi wa bidhaa, malighafi na mazao ndani na nje ya nchi. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na serikali yake, walijenga daraja kubwa mwaka 2003 likiunganisha Tanzania na Msumbiji kwa gharama ya Dola Mil. 30 ili kudumisha mahusiano mazuri ya kibiashara baina ya nchi hizo mbili.
Kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi/waajiriwa – Moja kati ya majukumu ya serikali ni kutetea haki za wafanyakazi wa sekta binafsi na za kiserikali ili kuondoa unyonyaji na ukandamizaji wa haki zao ikiwa ni pamoja na kupiga vita mazingira magumu sambamba na ulipaji wa ujira mdogo kwa wafanyakazi wa kampuni, shirika au taasisi inayojihusisha na biashara.
Ukusanyaji mapato na kodi – Hili ni moja kati ya jukumu kuu la serikali katika masuala yanayohusu biashara ambapo serikali imekuwa ikikusanya mapato na kodi kupitia TRA ili makusanyo hayo yasaidie katika utoaji huduma za kijamii sambamba na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu.
Kuondoa migogoro baina ya wawekezaji na wananchi – Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na idadi kubwa ya migogoro baina ya wawekezaji na wazawa hasa jamii za wakulima na wafugaji. Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa kusuluhisha migogoro hiyo ikiwa ni pamoja na kutafuta ukweli na ufumbuzi juu ya migogoro hiyo hasa inayohusu ardhi na viwanda. Mwaka 2016 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alifuta hati tano za umiliki wa ardhi katika maeneo ya Mwanza, Simiyu na Tabora zilizokuwa zinamilikiwa na Hamant Patel, raia wa Uingereza anayeishi Mwanza kinyume cha sheria na taratibu za nchi.
Kuhakiki ubora wa huduma na bidhaa kwa watumiaji au walaji – Moja kati ya kazi muhimu za serikali katika biashara ni kuhakikisha ubora na usalama wa huduma na bidhaa kwa walaji au watumiaji. Kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Serikali imekuwa ikifanya uhakiki na ubora wa bidhaa pamoja na ukaguzi wa kushtukiza katika maduka na viwanda mbalimbali nchini, Huku bidhaa ambazo hazina viwango vya kutosha zikipigwa marufuku sokoni sambamba na kuhakikisha zinateketezwa ili zisiendelee kusambazwa na kuleta madhara kwa watumiaji au walaji. TFDA pia imekuwa ikiwahakikishia usalama walaji na watumiaji wa vyakula, vipodozi na dawa juu ya habari za uzushi ambazo zimekuwa zikisambazwa mitandaoni kwa kutoa taarifa sahihi na kuondoa hofu miongoni mwa wananchi.
Hivi karibuni, TFDA ilitoa taarifa rasmi juu ya taarifa zilizokuwa zikisambazwa mitandaoni kuhusu dawa ya paracetamol (Panadol) kubadilika kuwa kitambaa pale inapomwagiwa maji, taarifa ambayo ilikanushwa na TFDA kwa kudai si taarifa ya kweli na inatakiwa kupuuzwa
Yaliyojadiliwa hapo juu ni kati ya majukumu muhimu ya serikali katika suala zima la uendeshaji wa biashara ndani ya nchi na nje ya mipaka yake. Ukuaji wa uchumi na biashara hautegemei serikali tu, bali hata mwananchi wa kawaida nae analo jukumu katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakua.
Haya ni baadhi tu ya majukumu ya mwananchi katika kuunga mkono serikali na kukuza uchumi, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi na ushuru kwa wakati, kuhakikisha ubora wa huduma na bidhaa anayotoa, kutafuta njia sahihi za kuondoa migororo baina yao na wawekezaji, kufuata hatua zote kisheria katika kupata vibali vya kuanzisha biashara, kuepuka rushwa sambamba na kutetea haki za wafanyakazi wenzake na jamii kwa ujumla.