Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano la TTCL, Waziri Kindamba amesema shirika hilo linatarajia kuanzisha mfumo ambao utamuwezesha mkulima kutafuta masoko moja kwa moja nje na ndani ya nchi kupitia simu yake ya mkononi ikiwa ni sehemu mojawapo ya utekelezaji wa mkakati wa serikali wa kuwezesha wakulima kutatua changamoto mbalimbali, ikiwemo ya ukosefu wa masoko.
Kindamba amedai wamefikia uamuzi huo kutokana na ushauri waliopata kutoka kwa Rais John Magufuli.
“Katika hafla ya kutoa gawio ambalo sisi tulitoa Sh. 1.5 bilioni, Rais aligusia kwa kusema nchini Ethiopia wakulima walio shambani wanaweza kuwasiliana moja kwa moja na masoko yaliyopo duniani. Hiki ndicho tunakifanya. Ushauri wa Rais ni maelekezo kwetu”. Ameeleza Kindamba.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa, mfumo huo utamsaidia mkulima kuona masoko na bei ya mazao na kisha kufanya ulinganifu na kuchukua uamuzi sahihi.
“Itamsaidia mkulima kufanya uamuzi sahihi ni wapi auze na katika muda gani. Wakati mwingine utakuta wakulima wanashindwa kuuza kwa kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi,” Amesema Kindamba.
Mkurugenzi huyo pia ameweka wazi kuwa TTCL inafanya kazi kwa karibu na wizara yenye dhamana na kilimo na kuongeza kuwa, mfumo huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa sio tu kwa wakulima bali kwa taifa zima kwa ujumla kwani wakulima watapata nafasi ya kuuza mazao yao kwa thamani halisi na kuondokana na ukandamizaji wa watu wa kati.