Serikali wilayani Hai mkoani Kilimanjaro imeombwa kuchukua hatua madhubuti kuokoa soko la mboga za majani kwa kuwapatia wakulima masoko ya uhakika pamoja na maeneo mazuri kwa ajili ya uendeshaji wa kilimo hicho.
Inatajwa kuwa bei ya mboga hizo imekuwa ikishuka mara kwa mara hali inayopeleka wakulimahao kupata hasara ikilinganishwa na gharama za uzalishaji. Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa mbogamboga wilayani hapo Nice John amesema iwapo serikali itawasaidia kupata soko la uhakika na maeneo ya kutosha kwa ajili ya kilimo hicho, itawasaidia kujikwamua na umaskini.
Akijibu hoja na malalamiko ya wakulima hao, Meneja wa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi mkoani Kilimanjaro kupitia shirika linalolinda na kutetea haki za Wanawake (Kwieco), Stewart Nathaniel amesema serikali imeamua kuanzisha mradi huo baada ya kutambua jitihada kubwa inayofanywa na akina mama hao sambamba na kupokea kero za manyanyaso ambayo wamekuwa wakizipata katika familia.
Aidha Nathaniel alisema kuwa baada ya serikali kutambua uwepo wa fursa za kiutalii mkoani humo waliwahamasisha wanawake na kuwatafutia wataalamu wa kilimo ili kuwasaidia kujikwamua na kuwaahidi kuzitekeleza changamoto walizonazo kwa sasa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa soko la uhakika.