Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahene amewataka maofisa ugani wilayani Mpwapwa kuanza matayarisho ya daftari la wakulima kwa ajili ya maandalizi ya mashamba ya kilimo kwa kuwa msimu wa kuanza kufanya hivyo umekaribia. Dk. Mahene amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo ambapo amewataka maofisa hao kuwasaidia wakulima ili waweze kuzalisha mazao yanayoendana na mvua chache ya kati ya milimita 400 hadi 800 inayonyesha kwa siku 60 katika mkoa huo.
Mkuu huyo amesema baadhi ya faida za kuandaa daftari hilo mapema ni pamoja na kuwasajili wakulima na kutambua wanaofanya kazi na kuwa na kumbukumbu zao sahihi na kujua wanataka kuzalisha nini katika mwaka huu.
“Maofisa ugani elekezeni wananchi namna ya kuandaa mashamba, kupanda na kuzalisha kwa nafasi na aina ya mazao, kutumia mbegu bora na kutunza vema mazao yanayopatikana,” amesema”. Ameagiza Dk. Mahene.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri amesema wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa mkoa huku akiongeza kuwa, atahakikisha maofisa ugani wilayani humo wanasimamiwa na kuanzisha daftari la wakulima mapema ili kufahamu kiwango cha uzalishaji katika kaya zote za wilaya hiyo.