Home VIWANDANISHATI Mradi wa umeme kuokoa mabilioni

Mradi wa umeme kuokoa mabilioni

0 comment 96 views

Serikali kupitia Wizara ya Nishati inatarajia kupunguza gharama za ufuaji umeme kwa kuokoa kiasi cha fedha zipatazo Sh. 9.1 bilioni zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya kununua mafuta mazito. Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani katika hafla ya ukaguzi wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV220 kutoka Makambako mkoani Njombe hadi Songea, unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni baada ya Waziri huyo kuridhishwa na kiwango chake.

Akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu wake Subira Mgalu, Katibu wa wizara hiyo, Dk. Hamisi Mwinyimvua na watendaji wengine kutoka wizara ya nishati na Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Dk. Kalemani amesema serikali imekuwa ikitumia kiasi cha Sh. 9.1 bilioni kila mwaka kununua mafuta mazito yaliyokuwa yakitumika kuzalishia umeme katika mikoa ya Njombe na Ruvuma pamoja na wilaya 8 ambazo zilikuwa hazijaunganishwa kwenye umeme wa gridi ya taifa.

“Kukamilika kwa mradi huu ambao ulianza 2016, kutaondoa adha na gharama ua kutumia mafuta mazito katika kuzalisha umeme kwa maeneo yaliyokosa umeme wa gridi ya taifa kwa miaka mingi ukiwemo Ruvuma” Amesema Dk. Kalemani.

Aidha, Waziri huyo amedai serikali inatarajia kuzima mashine tano zilizokuwa zikitumia mafuta hayo ili maeneo hayo yaunganishwe katika gridi ya taifa, huku akitaja maeneo hayo kuwa ni Madaba, Mbinga, Namtumbo, Ludewa na Songea. Dk. Kalemani amewataka wakandarasi wa mradi huo kuunganisha vijiji vitatu kila wiki ili vijiji vyote viweze kunufaika na mradi huo ifikapo 2021.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mgalu amepongeza kukamilika kwa mradi huo na kumuagiza mkandarasi wa kampuni ya Isolux mwenye zabuni ya kusambaza umeme vijiji 122 kukamilisha kazi hiyo kwa wakati. Naye Kaimu Mkuu wa mkoa wa Njombe ameahidi kuusimamia mradi huo pamoja na miradi mingine inayotekelezwa mkoani humo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter