Mkaguzi kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Emmanuel Saimon amesema operesheni waliyofanya katika soko la Tandika jijini Dar es salaam imefanikiwa kuondoa tani zaidi ya moja ya nguo za ndani katika soko, ikiwa ni mkakati mojawapo wa shirika hilo kuhakikisha nguo hizo hazifiki mikononi mwa watanzania kutokana na madhara yake kiafya. Mkaguzi huyo amedai kuwa, TBS inalenga kulinda afya za wananchi hivyo wanaondoa nguo hizo katika mzunguko kutokana na madhara yake.
Saimon ametaja baadhi ya madhara ya nguo hizo kuwa ni pamoja na magonjwa ya ngozi ikiwemo kansa na kushauri wafanyabiashara waliojikita katika biashara hizo kuachana nayo mara moja ili kuepuka hasara. Amefafanua kuwa zoezi hilo litaendeshwa nchi nzima na utekelezaji wake ni kwa mujibu wa Sheria ya Viwango ya mwaka 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani za mitumba.
“Licha ya unafuu wa gharama za upatikanaji wa nguo za mitumba nchini, serikali kupitia shirika letu imepiga marufuku biashara ya uuzwaji wa nguo hizo, ikiwemo soksi, sidiria na nguo za kulalia kwa sababu zina madhara kwa mtumiaji”. Amesema mkaguzi huyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi walioshuhudia tukio hilo wameonyesha kuunga mkono zoezi la shirika hilo wakisema japokuwa bei ya bidhaa hizo ni nafuu, madhara yake ni kiafya ni makubwa.