Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la siku tatu la wakulima wapatao 2,400 kutoka maeneo mbalimbali nchini. Kongamano hilo litakalofanyika katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro Oktoba 3 linaadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa taasisi ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata).
Akizungumza na waandishi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mviwata, Stephen Ruvuga amesema Waziri Mkuu atafungua maadhimisho hayo na atapata nafasi ya kufanya mazungumzo na wakulima hao. Ruvuga ameongeza kuwa, kongamano hilo litaambatana na kongamano la kitaifa la wakulima kuhusu ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Akielezea kuhusu kongamano hilo, Ruvuga amesema kutakuwa na majadiliano kuhusu jinsi gani wakulima wanaweza kujipanga na kuwa washiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda pamoja na kuangalia nyenzo muhimu za kufanikisha ushiriki wa wakulima wadogo katika mfumo wa uchumi wa viwanda ikiwa ni mkakati wa serikali ya awamu ya tano
Watu mbalimbali wanatarajia kushiriki katika kongamano hilo wakiwemo mawaziri, wabunge, viongozi na watendaji waandamizi, Kamishna wa ardhi, wawakilishi wa balozi, Prof. Issa Shivji, washirika wenza, marafiki wa Mviwata na wadau wengine wa kilimo kutoka ndani na nje ya nchi.