Baada ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kuwaamuru wamachinga ambao wamejenga vibanda vyao kuzunguka soko la kimataifa la Mwanjelwa kubomoa vibanda hivyo na kuondoka katika eneo hilo na kuhamia katika eneo la Nanenane ambalo tayari lina vibanda zaidi ya 700 vilivyojengwa maalum kwa ajili yao, wafanyabiashara hao wadogo wamegomea agizo hilo na kuleta vurugu ikiwemo kufunga barabara.
Baadhi ya wafanyabiashara hao wamedai kuwa eneo hilo walipewa na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla kwa ajili ya kujenga vibanda na kufanya biashara zao baada ya kuwaondoa katika hifadhi ya barabara lakini wameshangazwa na uongozi wa hivi sasa kutaka kuwaondoa.
“Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wetu kabla ya Chalamila ndiye aliyetuweka hapa, sasa tunashindwa kuelewa kwa nini tuondoke, sisi hatutaki kuondoka, kwanza sisi huyu mkuu wa mkoa hatumtaki”. Alisikika akisema mmoja wa wafanyabishara hao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wamachinga hao Jerry Mwatebela amesema kitendo cha wafanyabiashara wenzake kufanya fujo pasipo yeye kujua kimesikitisha kwani tayari viongozi wanashughulikia suala hilo. Mwatebela ametoa wito kwa wamachinga hao kutulia wakati wakisubiri majibu ya barua yao kutoka Ofisi ya Rais.