Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli ameihakikishia serikali ya Misri kuwa serikali ya awamu ya tano itasimamia utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) kwani mradi huo ni njia sahihi ya kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Rais Magufuli amesema hayo wakati akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi huo Ikulu jijini Dar es Salaam, zoezi lililoshuhudiwa na Waziri Mkuu wa Misri, Dk. Mostafa Madbouly.
Rais Magufuli ameeleza kuwa serikali yake ipo imara na itahakikisha mradi huo unaotarajiwa kuzalisha Megawati 2,100 unakamilika kwa wakati ili kuiwezesha Tanzania kuweza kupiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo. Rais Magufuli amesema imekusudia kuharakisha utekelezaji wa mradi wa Stiegler’s Gorge kutokana na kwamba, uzalishaji wa umeme kupitia chanzo cha maji ni rahisi ukilinganisha na vyanzo vingine vya uzalishaji wa nishati ya umeme ikiwemo upepo, makaa ya mawe, nyuklia, jua na joto ardhi.
“Ukiutazama mradi huu wa Stiegler’s Gorge unatoka katika mikoa na maeneo ambayo yana kiasi kikubwa cha mvua, lakini pia umeme wa maji ni rahisi sana ni Tsh 36 kwa uniti moja ukilinganisha na Nyuklia (Tsh 65), Jua (Tsh 103.5), joto ardhi (Tsh 114.5), upepo (Tsh 103.5), Makaa ya Mawe (Tsh 118), na mradi huu ukikamilika bei ya umeme itashuka kwa kiasi kikubwa sana”. Amesema Rais Magufuli.
Kuhusu tuhuma kutoka kwa baadhi ya makundi ya watu kuwa mradi huo utaleta tishio la uharibifu wa mazingira katika hifadhi ya Selous, Rais Magufuli amesema jambo ambalo halina ukweli wowote.
“Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na timu ya watalaamu wa serikali, hakutokuwa na athari yoyote ya mazingira na kwa kuwa mradi wote unachukua asilimia 1.8 ya eneo la hifadhi, lakini eneo lile litakuwa eneo mahususi kwa wanyama, ndege na viumbe wote wa majini ikiwemo kuongezeka kwa mazalia ya samaki”. Ameeleza Rais Magufuli.