Home FEDHA Dk. Mpango ashauri taasisi za umma kutumia GePG

Dk. Mpango ashauri taasisi za umma kutumia GePG

0 comment 38 views

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ametoa wito kwa taasisi za umma kuwa na akaunti za makusanyo kwenye benki zaidi ya moja kati ya benki zilizoungwa na Mfumo wa Serikali wa Ulipaji wa Kielektroniki (GePG) ili kuwarahisishia walipaji wa huduma za serikali. Dk. Mpango amesema hayo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa watumiaji wa mfumo wa GePG katika ukusanyaji wa fedha za umma ambapo amesema kuwa, utaratibu wa malipo kupitia GePG ni fursa ya kuwa na njia nyingi za kulipia fedha za umma.

“Kwa kuwa malipo yote yanayopitia GePG hayatozwi ada za miamala na benki hizo hivyo kuongeza akaunti za makusanyo katika benki hakutoongeza gharama za miamala kwa taasisi za umma bali kufanya hivyo kutaondoa hatari ya ofisi husika kukosa huduma ya malipo endapo benki inayotumika itashindwa kutoa huduma kwa sababu mbalimbali”, alisema Dkt. Mpango.

Dk. Mpango amefafanua kuwa utaratibu huo unaenda sambamba na utekelezaji wa maagizo mengine ya serikali kuhusu makusanyo ikiwemo yale yanayotaka akaunti kuu za makusanyo za taasisi za umma kuwepo Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Aidha, Waziri huyo amezikumbusha taasisi ambazo hazijajiunga na mfumo wa GePG hadi sasa kuwa ifikapo Juni 30 mwakani, hakutokuwa na fedha yoyote ya umma itakayokusanywa nje ya mfumo huo.

Katika maelezo yake, Waziri Mpango amesema mfumo huo unachochea ubunifu katika kukusanya fedha za serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya usawa kwa wakusanyaji, kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za umma pamoja na kusaidia fedha kufika haraka katika akaunti kuu za makusanyo za taasisi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter