Halmashauri ya Rungwe mkoani Mbeya imetoa mkopo wenye thamani ya Sh. 74.9 milioni kwa vikundi 13 vya wanawake na vijana ili kuchochea shughuli za ujasiriamali wanazofanya ikiwa ni utekelezaji wa sera ya nchi inayoelekeza Halmashauri nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vikundi vya wanawake, vijana pamoja na wale walio na ulemavu.
“Sera inataka kuwepo na uwezeshaji wananchi kiuchumi mpaka kufikia mwaka 2030, hivyo sisi kama Halmashauri tutaendelea kutekeleza mpaka tuhakikishe wananchi wetu wanainuka kiuchumi na wanakuwa na uwezo wa kuendesha maisha yao”. Amesema Deodatus Nenze, Ofisa Maendeleo ya Jamiii wa Wilaya ya Rungwe.
Kwa upande wao,baadhi ya wajasiriamali walionufaika na mkopo huo wamesema fedha hizo zitasaidia kukuza uchumi wao kwa kuongeza mitaji katika biashara wanazofanya. Pamoja na hayo, wajasiriamali hao pia wametumia fursa hiyo kueleza changamoto mbalimbali ambazo bado wanakumbana nazo kama vile ukosefu wa elimu ya ujasiriamali na mfumuko wa bei za bidhaa.