Home BENKI Blockbonds, I & M wazindua SPENN

Blockbonds, I & M wazindua SPENN

0 comment 109 views

Kampuni ya Blockbonds ya nchini Norway na benki ya I & M wamezindua huduma mpya ya SPENN inayolenga ili kuwapa urahisi watanzania kufungua akaunti binafsi au ya biashara kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kumuwezesha mtumiaji kutuma na kupokea fedha bila makato yoyote.

Katika hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo iliyofanyika jijini Dar es salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Blockbonds na SPENN, Jens Glaso ameelezea kuwa huduma hiyo ni ya kila mtanzania na kwamba mtumiaji anaweza kupata huduma ya kuweka na kutoa fedha bila gharama katika benki ya I & M sehemu yoyote nchini na vilevile katika maduka mbalimbali .

“Huduma imeanza kupatikana Tanzania na nchi za Afrika, mwaka jana tuliweza kuizindua nchini Rwanda na tayari kuna watumiaji zaidi ya 130,000 ambao wameshajiunga”. Amesema Mtendaji huyo.

Pamoja na hayo, pia ameeleza kuwa, dhumuni la kuanzisha huduma hiyo ya uhakika na rahisi ni kumfikia mtanzania yeyote asiye na akaunti ya kuhifadhi fedha ili aweze kuweka akiba na kuwataka wafanyabiashara nchini kufanya mauzo ya bidhaa zao na wateja kulipa kupitia SPENN badala ya kulipa fedha taslimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa I & M, Baseer Mohammed amesema benki hiyo inawekeza zaidi katika huduma za kidigitali, na SPENN  inalenga kukidhi mahitaji ya wateja.

“Huduma hiyo inayobadilisha namna ambavyo watanzania wanafanya miamala yao ya kifedha na kufanya mfumo mzima wa kufanya miamala kuwa na ufanisi zaidi, wenye usalama na pasipo kuwa na gharama, vilevile tunaamini kabisa huduma ya SPENN itachangia katika kuboresha maisha ya watanzania”. Amesema Mohammed.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter