Wakulima wa zao la korosho mkoani Mtwara wameomba Bunge kuingilia kati suala ya malipo yao kuchelewa huku wakidai kuchoshwa na matamko ambayo yanakosa utekelezaji. Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, wakulima hao wamedai tayari serikali imetoa maagizo kwa watendaji kuwalipa fedha hizo lakini utekelezaji wake bado ni sintofahamu.
Wakulima hao kutoka wilaya za Newala na Tandahimba wameliomba Bunge kushinikiza serikali kuwapatia fedha zao ili waweze kutatua changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo madeni na maandalizi kwa ajili ya msimu ujao.
“Tandahimba tuna tatizo la fedha. Watu hawajalipwa fedha zao. Tunataka fedha zetu, wakulima walipew fedha zao. Hatupati fedha za maendeleo hata za kwake asipate? Tatizo lipo wapi kama Rais aliagiza tulipwe, Waziri Mkuu aliagiza tulipwe, lakini bado wakulima hatulipwi. Kwa kuwa Kamati ya Bunge imefika, tunaomba Bunge lisimamie wakulima tulipwe fedha zetu”. Amesema mmoja wa wakulima hao
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Namkulya Suleiman Namkulya amesema pamoja na wakulima kutolipwa fedha zao, kukosekana kwa mapato ya ushuru pia kumeathiri Halmashauri hiyo.
“Asilimia 95 ya mapato yetu ya ndani yanategemea korosho, asilimia tano inategemea mnyororo wa thamani ya korosho, hivyo asilimia 100 tunategemea korosho hapa tulipo hakuna hata mradi mmoja unaotekelezwa kwa fedha za ndani. Tunaomba Kamati na Mheshimiwa Waziri mliangalie hili, Halmashauri tulipwe ushuru wetu unaotokana na korosho”. Amesema Namkulya.