Mkandarasi wa kampuni ya Jiangsu Etern Co. Ltd wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) amepewa siku 15 na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, kuhakikisha kuwa anawasha umeme katika kijiji cha Ruhita, wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
“Serikali inampa siku 15 mkandarasi kuhakikisha anawasha umeme katika kijiji chenu na kuripoti kila siku asubuhi katika ofisi ya Mwenyekiti wa kijiji, lengo ni kwenda kwa kasi”. Amesema Waziri Kalemani.
Waziri huyo amewaambiwa wananchi wa kijiji hicho kuwa nishati ya umeme ni muhimu katika maendeleo ya kijiji huku akiwasisitiza kuweka umeme kabla ya mwezi Julai mwaka huu, ambapo anategemea kufanya ziara nyingine ya ukaguzi wa maendeleo.
Vilevile ameongeza kuwa ni ruksa kwa wananchi kulipa gharama za umeme kwa awamu kwa kiasi cha Sh. 27,000 hadi pale watakapomaliza malipo hayo huku akiwaonya wale ambao hawatokuwa na umeme kuwa, watalazimika kuuza mifugo yao ili waweze kuwekewa nishati hiyo.
“Mradi wa Rea hauna fidia kwa wananchi hivyo niwaombe wananchi kutoa maeneo yao kupitishia nguzo za umeme kwani ni kwa manufaa yao na hazitumii eneo kubwa”. Amesema Dk. Kalemani.