Kamishna Mkuu wa Udhibiti wa Fedha Haramu Tanzania, Onesmo Makombe amezitaka nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika kutafuta suluhisho la fedha haramu ambalo limekuwa likiendelea kukua kwa kasi katika ukanda huo. Kamishna huyo amesema hayo wakati akifungua mkutano wa maofisa wa kupambana na fedha haramu jijini Arusha na kuongeza kuwa fedha haramu zimekuwa kikwazo kikubwa kupata maendeleo na hali hiyo imepelekea uchumi katika nchi hizo kuendelea kushuka.
“Serikali za nchi wanachama zinatakiwa kukabiliana na biashara haramu za binadamu, dawa za kulevya, rushwa na mengineyo yanayofanana na hayo, kwani mambo hayo ndiyo yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa fedha haramu”. Amesema Kamishna Makombe.
Ameshauri nchi wanachama kuwa na Sheria kali ambazo zitawabana wale wanaofanya shughuli hizo na kusisitiza kuwa endapo hatua makini hazitachukuliwa, uchumi wa nchi hizo utaendelea kudorora.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu Tanzania, Eliamani Kisanga amesema kupitia mkutano huo, nchi wanachama zitajadili Sheria ambazo zitasaidia kutatua tatizo hilo.
Mkutano huo unategemea kuchukua muda wa kwa wiki moja, ukishirikisha nchi wanachama takribani 18 ambapo wajumbe zaidi ya 200 wamehudhuria.