Home BIASHARABIASHARA NDOGO NDOGO Tumia mbinu hizi kukuza biashara yako

Tumia mbinu hizi kukuza biashara yako

0 comment 109 views

Ni kawaida kujiwekea malengo mbalimbali punde tu unapoanzisha biashara. Lengo moja ambalo sio geni kwa mfanyabiashara yoyote ni kuteka soko na kukuza biashara yake baada ya muda fulani. Japokuwa mazingira ya kufanya biashara hutofautiana kulingana na bidhaa au huduma inayotolewa, mbinu unazoweza kutumia kujiimarisha hufanana.

Kabla ya kuwekeza kwenye biashara ni vizuri kuwa na mpango ambao utakuongoza na kukusaidia kukufikisha pale unapotaka. Ni kweli kwamba kuna changamoto nyingi kwenye sekta hii kama ilivyo kwenye sekta nyingine. Kama mfanyabiashara mwenye malengo ni muhimu kutokata tamaa na kufanya kazi kwa bidii ili kuwa katika nafasi nzuri zaidi sokoni na kuendelea kuwavutia wateja kununua bidhaa zako.

Zifuatazo ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza kuzitumia kila siku ili kukuza biashara yako:

Uza bidhaa yenye mashiko

  • Ili wateja wamiminike unatakiwa kuwa na kile wanachohitaji. Huwezi kuuza mwavuli msimu ya jua kali kwani hakuna atakayenunua. Kama mfanyabiashara, ni muhimu kusoma soko lako siku zote na kuwapatia wateja kile wanachohitaji na sio vinginenyo. Ukiwa na bidhaa ambayo uhitaji wake kwenye soko ni mkubwa lazima watu wanunue.

Bei ziendane na uhalisia

  • Baadhi ya wafanyabiashara wamejikuta wakidorora kutokana na maamuzi yao ya kuuza bidhaa kwa gharama kubwa ambayo asilimia kubwa ya wateja wanashindwa kumudu. Wakati unapangilia bei, ni vizuri kuweka akilini nani hasa ni soko lako. Jiulize katika mazingira uliopo, utapata wateja wangapi kwa bei hiyo? Hakuna mtu atakayetumia kiasi kikubwa cha fedha kupata bidhaa ambayo wafanyabiashara wengine wanauza kwa bei rahisi na rafiki zaidi.

Kuwa mpambanaji

  • Kama unamiliki biashara au unafikiria kuanzisha biashara hupaswi kuwa mzembe. Unatakiwa kuwa tayari kutoa huduma bora kwa wateja wako muda wote. Kuwa tayari kumshauri mteja, kumuelekeza pale ambapo anapata wakati mgumu kuelewa na kuwa mtu ambaye ambaye yupo tayari kutoa msaada kwa wateja wake pale wanapohitaji. Usiwe mfanyabiashara ambaye anakaa tu dukani akitegemea wateja watamfuata pasipo ushawishi wowote.

Geuza wateja kuwa marafiki

  • Hii itajenga mahusiano ambayo kimsingi yatakufaidisha wewe. Ukiwa na wateja wa muda mrefu, wateja hao hugeuka kuwa marafiki. Uaminifu wao kwenye bidhaa na huduma zako utawafanya warudi kwako mara zote pale wanapohitaji kitu. Hili ni jambo zuri kwa mfanyabiashara kwani ni uwanja mzuri wa kupanua soko. Unaweza kuwaomba wateja hao watangaze biashara yako kwa marafiki zao kupitia mitandao ya kijamii na hata wanapokuwa nyumbani.

Usikate tamaa

  • Kuna wakati mambo yatakuwa magumu. Mipango yako haitoenda kama unavyotaka na hali hii huenda ikakuvunja moyo na kukufanya ukose motisha ya kufanya kazi kwa bidii. Hutakiwi kukata tamaa, jitahidi kujifunza kutokana na makosa, omba ushauri kutoka kwa wafanyabiashara wenngine au hata wataalamu. Changamoto mbalimbali ambazo zipo kwenye shughuli zako zisikuvunje moyo. Endelea kujituma na baada ya muda mambo yote yataenda sawa.

Ili kuwa na biashara yenye mafanikio, hakikisha unafuata mbinu hizi kila siku. Pamoja na hizo, kuwa na tabia ya kusikiliza wateja, kupokea ushauri na maoni yao. Wekeza katika kutoa huduma bora na kuwa mfuatiliaji wa huduma au bidhaa ambazo zina uhitaji mkubwa sokoni. Lengo kubwa la biashara sio tu kutengeneza faida, ni kupata wateja na kuwashawishi kurudi kwako kwa mara nyingine.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter