Home AJIRA Zingatia haya kabla hujasaini mkataba

Zingatia haya kabla hujasaini mkataba

0 comment 115 views

Mara nyingi watu wengi huwa hawaoni umuhimu wa kusoma mkataba, labda kwa sababu ya furaha ya kupata kazi. Jambo hili linatakiwa kubadilika kwa sababu siku zote nyaraka za maandishi ni ushahidi tosha ikiwa jambo lolote litatokea mbeleni na kupitia mkataba ni rahisi kujua kama kazi inakufaa au la. Mikataba kazini imewekwa kwa ajili ya kuhakikisha mwajiri na mwajiriwa wananufaika, na kila kitu kinaenda sawa huku pande zote mbili zikiendelea.

Hivyo ukiwa unasoma mkataba hakikisha kuwa mambo yafuatayo yameainishwa katika mkataba wako.

Kazi yako na maelekezo

Kujua upeo wa kazi yako ni muhimu kwa sababu hapa mwajiriwa anaelekezwa majukumu yake kazini. Hivyo hakikisha maelekezo kuhusu cheo chako yameelezwa ipasavyo ili kuepuka kusaini mkataba ili hali unajua huwezi kufanya kazi hiyo, pia kwa kujua majukumu yako itaepusha kufanya shughuli zisizokuhusu na kufanya kazi nyingi zaidi kwa mshahara mdogo.

Mshahara na bonasi

Hapa unatakiwa kuangalia mshahara mliokubaliana, malipo yake yatafanyika kwa mtindo gani na vilevile mfumo wake. Katika kipengele hiki, motisha na faida mbalimbali huelezwa hapa kwa mfano, faida za afya, malipo ya gharama za usafiri, chakula, n.k.

Sababu zitakazokufukuzisha kazi

Kila sehemu huwa kuna sheria na kanuni ikiwa mtu atazivunja sheria hizo basi hatua mbalimbali huchukuliwa. Hivyo katika kipengele hiki unatakiwa kusoma kwa bidii vitu ambavyo hutakiwi kuvifanya kazini na hatua ambazo zinaweza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvunja mkataba. Kuna neno linaitwa ‘sole discretion’ kuwa makini nalo kwa sababu inamaanisha kuwa mwajiri ana mamlaka ya kukufukuza muda wowote bila hata ya kuongea na wewe, hivyo unaweza kujadili tena na muajiriwa kuhusu kipengele hiki ili muende sawa.

Tarehe ya kuanza na mwisho wa mkataba pamoja na muda wa kutoa taarifa

Ni muhimu kujua tarehe ya kuanza na mwisho wa mkataba wako na muda wa kujiandaa kuchukua hatua nyingine ili kama mwajiri amefurahishwa na ufanisi wa kazi basi mnaweza kufanya majadiliano zaidi kuhusu nafasi yako ikiwa ni pamoja na kusaini mkataba mpya.

Likizo na mambo ya ghafla

Mkataba unatakiwa kueleza kwa uwazi kabisa kuhusu likizo na mambo ya ghafla kama ugonjwa. Hivyo katika mkataba wako inatakiwa kuelezwa siku utakazo pewa kwa ajili ya likizo na katika muda gani kwenye mwaka. Inaelezwa kuwa kuna baadhi ya nchi mgonjwa hulipwa, na kuna kazi ambazo humlipa mfanyakazi akiwa likizo na nyingi haziwalipi wafanyakazi wakiwa kwenye likizo. Hivyo hakikisha unazingatia suala hili na ikiwa unataka kuongeza kitu basi ongea na mwajiriwa wako ili kujua kama mabadiliko yanaweza kufanyika. Pia ni vyema kujua sheria kuhusu jambo hili kabla hujaomba mabadiliko yafanyike.

Masaa ya kazi

Unatakiwa kuangalia kama unatakiwa kufanya kazi siku za mwishoni mwa wiki au jioni na kujua kama kuna malipo zaidi au la. Kwa sababu ukiachana na kazi kuna maisha binafsi ikiwa unaona utaweza kumudu masaa yaliyoweka basi unaweza kusaini mkataba ikiwa unaona itakuwa changamoto kwako basi unaweza kujadili na mwajiri wako ili kuepusha na usumbufu mbeleni.

Aidha unatakiwa kujua mambo ambayo hutakiwi kufanya ambayo yanaweza kuathiri kampuni au biashara husika. Kwa mfano kufanya kazi na kuwapa habari washindani kuhusu biashara au kampuni husika, kufanya kazi na wateja wa zamani, kuwapunguzia bei wateja bila ofisi kujua nk.

Ni muhimu kutambua kuwa mkataba umewekwa kwa malengo mazuri na si kukomoa upande wowote. Umakini wako ndio utakusaidia kufanya maamuzi sahihi na kufurahia kazi yako.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter