Leo, wafanyakazi wa Benki ya Dunia ofisi ya Tanzania wakiongozwa na Mkurugenzi wao, Bi. Bella Bird, wamefanya usafi kwenye fukwe za bahari eneo la Coco Beach jijini Dar Es Salaam.
Usafi huo ulifanyika kama jitahidi za Benki ya Dunia ofisi ya Tanzania kuunga mkono mpango wa serikali kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo ilikua ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira.
“Ujumbe wetu kwa jamii ni wawe na wajibu wa kuepuka uchafuzi, kuondoa utamaduni wa kutupa taka ovyo na kua na tabia ya kuchakata. Tumefurahi Serikali imechukua hatua kubwa kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki na tunatumaini wataendelea kudhibiti”,alisema Bi.Bird.
Aliendelea kusema kwamba upunguaji wa taka za mifuko ya plastiki hakika ni kitu kikubwa kwa Tanzania kusherehekea. Pia alisema hatua itayofuata ni kupiga marufuku mirija ya vinywaji kwa kua haina matumizi yoyote muhimu kwa karne hii.
Nao wafanyakazi wa Benki ya Dunia ofisi ya Tanzania walisema kila mmoja ana jukumu la kutunza mazingira.
“Wote tunajukumu kwenye hizi taka. Makampuni ya vyakula na vinywaji yashiriki kutoa elimu kwa jamii, kupanga usafi, kuweka pipa za taka na kusaidia uzoaji taka kama jukumu la kampuni kwa jamii”,walisema wafanyakazi hao.
Nae, Carlos Mdemu ambaye ni mratibu wa ‘Nipe Fagio’ alisema “kuweka pipa za taka maeneo ya fukwe na mtaani ni mpango mzuri, lakini kwenye baadhi ya maeneo tumeona mapipa yanajaa na hakuna anayekuja kuyazoa, kwahiyo watu wanabidi wajue majukumu yao pia”.
Mdemu aliendelea kusema “kuwatoza faini kwa kutupa taka ovyo inafanywa na Manispaa ya Ilala na ni nzuri. Lakini kuongeza ufahamu inaweza kua muhimu zaidi ili kwamba watu wengi wakiwa wanajua, unapunguza nguvu ya kuwatoza faini”.
Kuhusiana na taka za plastiki Mdeme alisema “kwa sasa, taka yenye changamoto tuliyoona ni chupa za plastiki zenye rangi na vifungashio vya chakula (aiskrimu n.k). Chupa za plastiki za rangi hazikusanywi kwa ajili ya kuchakata kwasababu hazina soko kwa wakusanyaji”.
“Hapo nyuma tulipofanya usafi wa fukwe, tuligundua hesabu za taka za mifuko ya plastiki ni zaidi ya asilimia 50. Hii imebadilika, leo tumekusanya si zaidi ya asilimia 10” alisema Carlos Mdemu.
Wakihitimisha usafi katika fukwe za Coco Beach wafanyakazi hao walisema “tumeacha alama ndogo ukilinganisha na kinachotakiwa kufanywa. Lakini hii ndiyo sababu kwanini tumefanya na kwanini wote inabidi tuunganishe mikono na kuacha alama kubwa zaidi.
“Tunatekeleza tunachokisema, Benki ya Dunia Tanzania tunasema hapana kwa plastiki, weka fukwe na bahari yetu safi, sema hapana kwa matumizi ya plastiki, saidia mapambano dhidi uchafuzi wa plastiki” walisema wafanyakazi hao.