Home FEDHA Njia za kuepuka utapeli mtandaoni

Njia za kuepuka utapeli mtandaoni

0 comment 112 views

Imekuwa ni kawaida kusikia mtu ametapeliwa fedha mtandaoni. Kwa bahati nzuri au mbaya, teknolojia mpya zinazoendelea kuboreshwa zimewarahisishia wezi kuendelea kutapeli watu kila siku mwaka hadi mwaka kwa njia mbalimbali ambazo mara nyingi mtu hawezi kushtuka kuwa anatapeliwa.

Unaweza kuepuka tatizo hili kwa kufanya yafuatayo:

Usitume fedha kwa mtu usiyemfahamu

Ni muhimu kuhakikisha unatuma fedha kwa mtu unayemfahamu. Siku hizi kuna ujumbe mfupi ambao hutumwa ukieleza utume fedha katika namba husika. Mtu anaweza kusema kuwa hawezi kutapeliwa kwa mtindo huo lakini hii inawezekana, fikiria umetoka kuongea na simu na mtu mmekubaliana umtumie fedha baada ya kukata simu unapokea ujumbe unaosema “Zile fedha tuma kwenye namba hii”, kwa haraka unaweza kufikiria kuwa yule mtu uliyetoka kuongea naye amekuelekeza utume fedha kwenye namba mpya.

Ni muhimu kuhakikisha taarifa  zote ikiwa unataka kufanya muamala wa kutuma fedha. Katika kudhibiti wizi wa namna hii, Jeshi la Polisi nchini limechukua hatua ya kuwaonya wananchi na matapeli kupitia ujumbe mfupi wa simu.

Usitoe taarifa zako za kifedha

Kamwe usitoe taarifa binafsi za kifedha kwa mtu au biashara usiyoitambua. Taarifa zako binafsi zinapaswa kuwa siri ili kulinda fedha zako kwani zitakapowafikia matapeli ni rahisi kwao kuhamisha fedha zako pasipo wewe kujua.

Usibonyeze viungo vya maandishi (hyperlinks) katika barua pepe

Pale unapopata barua  pepe kutoka katika kampuni usiyoifahamu ikikuelezea kuwa ubonyeze viungo vya maandishi au ufungue kiambatanishi halafu uweke habari zako za kifedha, futa barua pepe hiyo moja kwa moja hata kama inaonyesha imetoka katika benki yako au kampuni yako ya mkopo.

Nywila (password) yenye nguvu ni muhimu

Siku zote huwa inashauriwa kutumia nywila ambayo utaikumbuka. Lakini kwa usalama zaidi unashauriwa kuunda nywila yenye nguvu na salama ili kuepusha wachuuzi kufikia taarifa zako kwa urahisi. Jitahidi kutengeneza nywila zenye herufi kuanzia nane, zenye herufi ndogo na kubwa ili kutengeneza nywila yenye nguvu na salama vilevile ambayo utaikumbuka kila wakati unapokuwa unahitaji kutumia.

Usitoe namba ya usalama wa jamii

Ikiwa unapokea barua pepe au umetembelea tovuti ambayo inauliza nambari yako ya usalama wa jamii, usiitoe. Kwa kuitoa unatakiwa kujiandaa kutapeliwa. Biashara halali mara nyingi huwa haziulizi habari hii.

Weka ulinzi katika kompyuta yako

Jenga mazoea ya kuweka antivirus, firewall, spyware n.k katika kompyuta yako ili kuhakikisha nyaraka zako zote muhimu zipo salama. Pia hakikisha programu zako zote hazijaisha muda wake wa matumizi.

Usifanye manunuzi kwa wafanyabiashara wasiojulikana

Ikija kwenye suala la biashara za mtandaoni jitahidi kutofanya biashara na kampuni ambazo hazifahamiki. Ikiwa unataka kufanya biashara na kampuni usiyoijua basi fanya utafiti kwanza ikiwa ni pamoja na kuangalia mrejesho, malalamiko yanayohusu kampuni husika.

Hakikisha tovuti unazotembelea ni salama

Kabla ya kuingiza maelezo yako ya kifedha kwenye tovuti yoyote, angalia mara mbili sheria za faragha za tovuti. Pia hakikisha tovuti hutumia encryption, ambayo kwa kawaida huonyeshwa katika upande wa kushoto. Unapoona hii ina maana kwamba mahali unapoingia ni salama.

Fanya utafiti

Ikiwa umepigiwa simu, umetumiwa ujumbe au umetumiwa barua pepe kuhusu masuala ya fedha, fanya utafiti ili kujua kama kampuni au mtu husika ni halali. Kwa kufanya ivyo itakuepusha kutuma fedha kwa matapeli.

Tambua kuwa mtu yoyote anaweza kutapeliwa muda wowote. Utapeli hufanywa mtandaoni na vilevile hata ana kwa ana hivyo ni muhimu kuwa makini na watu unaojihusisha nao.

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter