Home FEDHA Fedha zako zinaenda wapi?

Fedha zako zinaenda wapi?

0 comment 109 views

Sio kila mtu anayeshindwa kumudu gharama za mahitaji yake kwa mwezi huwa anapata mshahara au kipato kidogo. Kuna muda unaweza kuwa na kipato kizuri lakini bado ikawa changamoto kulipa gharama au kutatua masuala yanayotokea ghafla. Ifahamike kuwa kadri muda unavyokwenda, majukumu nayo huongezeka kwa namna moja au nyingine, hivyo ni muhimu kujua fedha zako zinakwenda wapi. Kujua tatizo hurahisisha mpango mzima wa kutafuta suluhu.

Baadhi ya maeneo ambayo unaweza kuangalia na kutathmini kama kuna tatizo ni haya hapa:

Makazi

Kila mtu hujisikia amani akiwa ana makazi mazuri na salama. Hivyo kipindi mtu akianza kutengeneza fedha zaidi lazima anatamani kupata sehemu nzuri yenye hadhi. Hakuna vitu vizuri visivyo na gharama hivyo kwa kupata sehemu nzuri zaidi lazima gharama zitaongezeka. Katika hali hii, unatakiwa kujiuliza je unatumia fedha kiasi gani kulipia makazi yako mapya?

Ikiwa inazidi asilimia 25 ya kipato chako unatakiwa kufanya mabadiliko kwa sababu kwa kulipa fedha nyingi katika sehemu unayokaa mahitaji mengine yanakosa fedha hivyo kupelekea kushindwa kulipa mahitaji mengine kwani unatumia fedha nyingi katika makazi.

Ikiwa hii ndio sababu inayofanya ushindwe kumudu mahitaji mengine basi jaribu kutafuta makazi yasiyo na  gharama kubwa ili kuokoa fedha na kuzielekeza katika mambo mengine.

Mikopo

Kuchukua mikopo sio jambo baya, lakini kuwa na mikopo mingi kunaweza kusababisha ushindwe kutimiza mahitaji yako hata kama una kipato kizuri. Jaribu kutathmini mikopo unayodaiwa, fedha unazotuma kila mwezi kwa ajili ya kulipa mikopo hiyo halafu linganisha na kipato chako ili kujua kama mikopo ndio sababu inayosababisha ushindwe kumudu mahitaji yako ili hali una kipato kizuri.

Ikiwa mikopo imezidi kwa asilimia 30 basi unashauriwa kutengeneza mpango kuilipa kwa haraka zaidi ili mambo mengine yaanze kwenda sawa. Kwa mfano unaweza kutafuta kazi ya muda mfupi ili kutengeneza fedha zaidi, au unaweza kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuokoa fedha.

Bajeti

Tatizo linaweza kuwa huna bajeti ya kufuata ndiyo maana fedha zako hazikidhi mahitaji. Bajeti ni zaidi ya orodha ya malipo unayotakiwa kulipa kwa mwezi, bajeti ni mpango unaokusaidia kufanya maamuzi ya jinsi utakavyotumia fedha. Hata kama una kipato kikubwa, bajeti ni muhimu . Kuwa na bajeti kutakusaidia kufuatilia gharama na kuweka kikomo cha matumizi yako.

Ni muhimu kutambua kuwa haitakuwa rahisi kufanya mabadiliko hivyo anza leo ili kuweza kumudu mahitaji na fedha zako kwa ujumla.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter