Home FEDHA Unakwama wapi kuongeza kipato chako?

Unakwama wapi kuongeza kipato chako?

0 comment 171 views

Imekuwa ni kawaida kuona watu hasa vijana wana kazi ya kuajiriwa na kazi nyingine ambayo wanaifanya baada ya kutoka kazini, inaweza kuwa kazi nyingine ya kuajiriwa kwa mfano katika migahawa ya chakula, katika maduka ya bidhaa nk au inaweza kuwa biashara binafsi ili kujipatia kipato zaidi.

Sio kila mtu huwa na ujasiri wa kufanya kazi zaidi ya moja ili kuongeza kipato na kutimiza malengo, kwasababu wengi wao huogopa hatari iliyopo katika kujihusisha na vyanzo vingi vya pesa kwa wakati mmoja huku wengine wakiwa na sababu zao binafsi.

Hivyo ikiwa unasita kuhusu kufanya kazi zaidi ya moja au kuanzisha sehemu nyingine ya kipato, basi maswali yafuatayo yatakusaidia kuondokana na uoga na kufanya mabadiliko.

Nitaanzaje?

Kuna njia nyingi za kutengeneza mtiririko wa mapato yako ya ziada. Unaweza kwa kufanya kazi sehemu mbalimbali siku za wikiendi au unaweza kuuza bidhaa mbalimbali kwa watumiaji kulingana na mahitaji. Pia ni muhimu kukumbuka kuwa kila mtu ana talanta yake aliyozaliwa nayo na mara nyingi kupitia talanta hiyo unaweza kujikuta unapata fedha kwa kuuza vitu au kutoa huduma inayotokana na talanta yako. Kuna vitu ambavyo kila mtu akifanya huvifanya kwa umahiri na bila shida yoyote hivyo unaweza kutumia fursa ya kutengeneza fedha kupitia vitu unavyofurahi kuvifanya. Kwa mfano kama unapenda kutengeneza keki, unaweza kutenga muda wa kufanya hivyo na kuuza kwa watu mbalimbali, hakikisha watu wanafahamu bidhaa yako hivyo unaweza kuanza na watu wa karibu kama ndugu, jamaa na marafiki ambao kwa namna moja au nyingine watakusaidia kukuza mtandao wa wateja hasa ukiwa una bidhaa au huduma ambayo watu wengi wanahitaji.

Inakuaje kuhusu ushuru na leseni?

Milolongo ya kulipa ushuru na kupata leseni huwakatisha tama wajasiriamali wengi kuanzisha biashara zao. Lakini kadri siku zinavyokwenda serikali inajitahidi kupunguza vikwazo vingi vilivyopo katika ushuru na leseni kwa wafanyabiashara nchini. Hivi sasa wajasiriamali wanaweza kujipatia kitambulisho kwa Shilingi 20,000 tu kwa mwaka ukilinganisha na zamani ambapo walikuwa wakisumbuliwa masuala ya ushuru kila wakati jambo ambalo limewafanya baadhi yao kufunga biashara zao.

Njia zipi ni rahisi za kuanzisha biashara?

Ni muhimu kuanzisha kitu ambacho ni rahisi kwako na kina faida kwa watu wengine. Kuna vitu vingI vya kawaida ambavyo watu huwa hawaoni shida kulipia kwa mfano watu hawana muda wa kupanga vitu vyao, kutokana na majukumu mengi hivyo ikiwa unapenda kupanga vitu katika mpangilio unaweza kuanzisha huduma hiyo na kujipatia fedha za ziada, kuna kampuni na wafanyabiashara wanohitaji wasimamizi wa mitandao ya kijamii,  kuna watu wanahitaji kujifunza lugha mpya hivyo kama una fahamu lugha zaidi ya moja  unaweza kuchangamkia fursa kama hizo.

Nitapataje muda?

Kazi ya ziada siku zote haihitaji siku nzima kuianza. Hivyo kama unaweza kutumia mitandao ya kijamii masaa kadhaa kwanini muda huo usiutenge kwaajili ya kufanya mambo yatakayokuingizia fedha zaidi ? Fanya maamuzi, jua mambo yapi ni muhimu ili kuweza kutumia muda wako vizuri.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter