Home AJIRA Biashara ya mtandao na changamoto ya utapeli

Biashara ya mtandao na changamoto ya utapeli

0 comment 188 views

Umewahi kuwaza kufanya biashara ya mtandaoni?. Biashara ya mtandao ni biashara inayokuwa kwa kasi.

Kwa sasa watu wengi wakiwemo vijana wamejikita katika biashara ya mtandao ili waweze kujikwamua kimaisha na kujipatia kipato.

Swala la ajira bado limekuwa changamoto ambapo vijana wengi wanahitimu elimu kwa ngazi mbalimbali lakini ajira zilizopo ni chache ukilinganisha na idadi ya wahitaji.

Licha ya kuwa teknolojia inakua kwa kasi na kurahisisha ufanyaji wa biashara kwa njia ya mtandao, biashara hii imekuwa na changamoto mbalimbali.

Baadhi ya wauzaji na wanunuzi wa mtandaoni wanakumbana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa kikwazo kwenye kukuza biashara zao.

Sarah Mushi ambae ni mfanyabiashara wa maua kwa njia ya mtandao anataja baadhi ya changamoto anazokutana nazo kuwa ni pamoja na muda.

“Wakati mwingine biashara hii inakuchukua muda mrefu sana katika kuwasiliana na mteja, kumshawishi mteja, kumtumia picha na uwe mtandaoni muda wote ili kungoja mrejesho wa mteja.

Wakati mwingine mnatumia siku nzima katika kufanya mazungumzo pekee kabla mteja hajafanya chaguo la bidhaa anayoitaka,” anaeleza Sarah.

Anaeleza kuwa mteja anatumia muda mwingi kumwamini muuzaji na kuielewa bidhaa kabla ya kuinunua.

“Unajua hii biashara inafanyika kwa njia ya mtandao, unapomtumia mnunuzi picha maswali yanakuwa mengi tofauti na kama mteja angekuja dukani au eneo la biashara na kujionea bidhaa, kwani wakati mwingine picha zinaweza kuongeza au kupunguza ubora wa bidhaa hususani kwa muonekano wa rangi,” anaeleza.

Anataja uaminifu kuwa changamoto nyingine katika biashara hii.

“Hapa ni kwamba kila mmoja hamwamini mwenzake linapokuja swala la kufanya malipo na kutumiwa bidhaa, huwa mteja anapaswa kufanya malipo kwanza ndipo atumiwe bidhaa yake, sasa wakati mwingine mteja anaogopa kutapeliwa na muuzaji anaogopa kutuma bidhaa kabla ya malipo.

“Kuna baadhi ya wafanyabiashara sio waaminifu na wanaharibu soko la biashara hii ya mtandao kwa kupokea pesa za wateja na baada ya hapo hawawatumii bidhaa zao na kufanya wote tuonekana matapeli,” anaeleza.

Lila Shopping ni mfanyabiashara wa mavazi ikiwemo nguo, viatu na urembo.

“Changamoto zipo nyingi ikiwemo ubora wa nguo kutokana na picha, ukubwa wa bidhaa na aina ya bidhaa.

Unaweza ukamtumia mteja picha ya bidhaa na akachagua lakini unapompelekea anasema sikujua kama ipo hivi picha iliing’arisha sana na hapa naona ni tofauti.

Hapo unakuwa umeshapoteza muda na gharama za usafirishaji na mteja anarudisha bidhaa, hiyo ni moja ya changamoto kubwa tunayokumbana nayo.

Akizungumzia swala la kuwepo kwa utapeli katika biashara hiyo anasema “ni kweli kuna watu wanatapeli, wauzaji na wateja wote wanaweza kufanya utapeli. Mimi niliwahi kupata mteja akanitumia pesa nikamtumia bidhaa, akanitafuta tena akihitaji bidhaa akanitumia pesa nusu kwa miadi kuwa atamalizia baada ya mzigo kumfikia, kwa kuwa nilishafanya nae biashara nilimwamini na kumtumia bidhaa lakini mpaka sasa hajanilipa na simu yangu hapokei tena.”

Amewataka wauzaji na wateja kuwa waaminifu katika ufanyaji wa biashara.

Alex Moleli ni mmoja wa wanunuzi kwa njia ya mtandao ambapo anasema uuzaji kwa njia ya mtandao unarahisisha manunuzi.

“Ukiingia mtandaoni unaona wafanyabiashara mbalimbali na unaweza kununua kitu unachokihitaji kwa urahisi na uharaka. Japokuwa wakati mwingine unaweza kununua kitu kikawa tofauti na ulivyokiona mtandaoni lakini biashara hii imerahisisha manunuzi, anaeleza.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter